Michezo

Macho kwa Ronaldo Juventus ikiendea Ajax

April 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

AMSTERDAM, Uholanzi

BAADA ya kupenya kiajabu kutoka hatua ya 16 bora, klabu za Ajax Amsterdam na Juventus zitakutana leo Jumatano usiku ugani Johan Cruyff Arena kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya kuwania ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA.

Timu hizo zitarudiana uwanjani Allianz Stadium nchini Italia kati ya Aprili 16 na 17 kwa pambano la marudiano.

Baada ya kushindwa na Real Madrid katika mkondo wa kwanza, Ajax walishangaza wengi kwa kuibuka na ushindi wa 4-1 katika mechi ya marudiano iliyochezewa Santiago Bernabeu.

Lakini kutokana na hali ya sasa ya kikosi cha Juventus kitakachomtegemea Cristiano Ronaldo, huenda wakatatizika.

Mechii hii imefika wakati Juventus wanajiandaa kubeba ubingwa wa Serie A kwa mara ya nane mfululizo.

Baada ya kuchapwa 2-0 na Atletico Madrid katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 bora, vijana hao wa kocha Max Allegri walisonga mbele kutokana na mabao matatu ya Ronaldo katika pambano la marudiano.

Aliyekuwa nyota wa Ajax Amsterdam, Jesper Olsen amesema uwepo wa kinda Frenkie de Jong kikosini utaiwezesha timu hiyo kuandikisha matokeo ya kuridhisha usiku huu.

Olsen alisema mchango wa staa huyo anayejianda kujiunga na Barcelona mwishoni mwa msimu utaiongezea nguvu safu ya kiungo ya kikosi cha kocha Erik ten Hag.

Mbali na Barcelona, kadhalika De Jong alikuwa akiwaniwa na klabu ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa kabla ya mwenyewe kuamua kujiunga na Barca kwa mkataba wa Sh12.9 bilioni.

“Kuna wachezaji wengi wazuri kote duniani ambao hung’ara kila wakati, lakini kiwango cha De Jong kipo juu zaidi licha ya umri wake mdogo,” alisema Olsen ambaye aliisaidia Ajax kutwaa mataji kadhaa alipowachezea miaka ya themanini.

Cristiano Ronaldo. Picha/ Maktaba

“Nafurahia ameamua kujiunga na timu ya hadhi ya juu. Barcelona na Real Madrid zitaendelea kuongoza kutokana na umaarufu wa wachezaji wao. Kwa mfano, Messi amevuma kwa zaidi ya miaka 10 hata baada ya umri wake kuendelea kusonga,” aliongeza.

Kuchangia upatikanaji magoli

De Jong amefunga mabao matatu msimu huu, licha ya kutoa mchango mkubwa katika kampeni za Ajax msimu huu, ukiwemo ushindi wao dhidi ya Real Madrid katika raundi ya 16 bora ya michuano ya Klabu Bingwa.

Ajax watamtegemea kipa Anana langoni, huku safu ya ulinzi ikimilikiwa na Tagliafico, Blind, De Ligt, Veltman, De Jong, Van de Beek, Schone, Neres, Tadic na Ziyet.

Juventus watakuwa na Szczesny, Cancelo, Bonucci, Rugani, Alex Sandro, Khadira, Pjanic, Matuidi, Bernardeschi, Manduzukic na Ronaldo.