• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MAUAJI YA WANGECHI: Daktari mtarajiwa alikuwa mwerevu chuoni, aeleza mhadhiri

MAUAJI YA WANGECHI: Daktari mtarajiwa alikuwa mwerevu chuoni, aeleza mhadhiri

JEREMIAH KIPLANG’AT, WYCLIFF KIPSANG NA DANIEL OGETTA

IVY Wangechi, mwanafunzi wa udaktari aliyeuawa kinyama mjini Eldoret Jumanne katika Chuo Kikuu cha Moi alipata alama ya ‘A’ katika mtihani wa KCSE.

Aliufanya mtihani huo wa kidato cha nne katika Shule ya Wasichana ya Alliance mnamo mwaka wa 2012. Akaupita na kisha kusajiliwa katika chuoni Moi, bewa la Eldoret kusomea udaktari.

Angelifika Desemba mwaka huu, angelihitimu kama daktari lakini maisha yake yalikatizwa asubuhi ya Jumanne na mwanaume ambaye polisi wamemtambua kama Naftali Kinuthia.

Kama waelezavyo wahadhiri wa chuo hicho, Ivy Wangechi, alikuwa mwanafunzi mwerevu ambaye nyota yake katika taaluma ya udaktari ilikuwa iking’aa.

Siku ya Jumatano, mhadhiri mkuu wa bewa hilo, Lukoye Atwoli alieleza Taifa Leo Dijitali kwamba Wangechi alikuwa mwanafunzi mtiifu na mwenye bidii.

“Japo matokeo ya kielimu ya kila mwanafunzi ni siri, Wangechi amekuwa akifanya vyema,” alisema Prof Atwoli.

Wandani wake Ivy ambao waliomba wasitajwe, walitueleza kwamba Bw Kinuthia alimpenda sana Ivy. Japo wakati mwingi angesafiri hadi Eldoret kumtembelea, Ivy angedinda kumpokea, jambo ambalo lilimghadhabisha sana Kinuthia.

Walisema kwamba Kinuthia angemsubiri Wangechi kwenye lango kuu la chuo hicho. Lakini, Wangechi angekataa abadan katan kumkuta.

Walizidi kutueleza kuwa Wangechi alibadilika na kuwa mnyamavu na msiri na kwa umbali, alionekana mwenye kusongwa na mawazo. Marafiki zake hawangeweza kuthibitisha ni jambo lipi linamtatanisha.

“Amekuwa mchangamfu na tumekuwa tukizungumza naye bila vizingiziti ila akabadilika wiki mbili zilizopita. Ningemtumia arafa fupi ila angejibu lisaa limoja baadaye,” mmoja wa rafiki zake alieleza.

Inasemekana kwamba Kinuthia alikuwa na uraibu wa kutuma pesa na wakati mwingine hata kutuma zawadi licha ya Wangechi kumkanya mara kadhaa dhidi ya kutuma.

Kwa sasa Kinuthia anapokea matibabu katika hospitali ya Moi mini Eldoret. Hii ni kufuatia  kichapo cha raia waliompiga kwa jiwe ili kumtia adabu lakini akaokolewa na polisi.

Mkuu wa Polisi wa Ainabkoi, Lucy Kananu alisema kwamba gari alilolitumia mshamulizi huyo ni la aina ya Honda lenye nambari la usajili KCB 836P na limenaswa na kuegeshwa katika kituo cha polisi cha Naiberi likusubii uchunguzi zaidi.

Bi Kananu ambaye pia alimtembelea hospitalini, alisema kwamba mshukiwa hawezi kuzungumza kutokana na maumivu yaliyotokana na kipigo alichokipata kutoka kwa umma.

“Akirejea katika hali ya kawaida, tutamhoji zaidi na kumwasilisha kortini kuwajibikia mauaji aliyotenda. Bado hatujajua nia yake ya kumshambulia Wangechi lakini tutabaini hivi karibuni. Pia tutajumuisha wandani wake Wangechi ili tuelewe kwa kina kilichotendeka, ” alieleza.

Prof Lukoye naye aliomba umma kutosambaza uvumi kuhusu chanzo cha mauaji ya Wangechi. “Ningependa kuomba wanaoandika na kusambaza uvumi kuhusu mauaji ya Wangechi kukoma,” akasema.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya lugha rasmi katika...

Maseneta wapinga mpango wa kupigwa marufuku kwa mbolea ya...

adminleo