• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Kuria aelezea kukerwa na malumbano ya Ruto na Raila

Kuria aelezea kukerwa na malumbano ya Ruto na Raila

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria amejitokeza kuwakejeli kinara wa chama cha ODM Raila Odinga na Naibu Rais Dkt William Ruto kwa kushiriki malumbano akisema hali hiyo inapandisha joto la kisiasa nchini.

Katika aliyotuma kwa vyombo vya habari Jumatano, Bw Kuria alielezea kusikitishwa na viongozi hao akisema wameghairi masilahi ya wananchi waliowachagua.

“Kwa mtazamo wangu viongozi wanafaa kushughulikia changamoto zinazowakabiliwa Wakenya kama vile ukame, njaa, ukosefu wa ajira, utovu wa usalama, bei duni ya bidhaa za kilimo, kuteswa kwa wakulima wadogo, kucheleweshwa kwa malipo na serikali ya kitaifa na zile za kaunti badala ya kutumia muda wao mwingi kulumbana,” akaandika Bw Kuria.

Mbunge huyo wa Gatundu Kusini aliendelea kuorodhesha masuala ambayo anahisi viongozi wanapaswa kuyapa kipaumbele badala ya kuchapa siasa.

“Inasikitisha kuwa Wakenya wanakabiliwa na shida ya barabara mbaya, ukosefu wa maji safi, umeme na huduma bora za afya. Familia nyingi haziwezi kumudu lishe mara tatu kwa siku,” akaendelea

Bw Kuria ansema kuwa inashangaa kuwa huku Wakenya wakikabiliwa na matatizo hayo wanaisiasa bado wanaweza kuendeleza malumbani kwa ajili ya kushindania mamlaka.

“Ningewaalika pande kinzani wajiulize ni kwa nini wao ndio wanaongea ilhali wengine wamenyamaza. Watu wetu wanawasoma na hivi karibu watasema imetosha,” akaongeza.

Haya yanajiri baada ya vita vya maneno kuibuka kati ya mrengo wa Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusu suala la muafaka wa maridhiano.

Akihojiwa katika runinga ya Citizen Jumanne usiku, Dkt Ruto alidai kuwa Bw Odinga alijaribu kufikia mara nne akitaka wafanye mazungumzo kabla ya kiongozi huyo wa ODM kukutana na Rais Uhuru Kenyatt kwa kile kilinachojulikana kama handisheki, mnamo Marchi 9, 2018.

Kauli hiyo ilichochea majibu makali kutoka kwa uongozi wa ODM huku katibu mkuu Edwin Sifuna akikana madai hayo na kudai ni Dkt Ruto aliyemfikia Bw Odinga akitaka wafanye mazungumzo kuhusu njama ya kujuhumu utawala wa Rais Kenyatta.

You can share this post!

KQ haina uwezo kutwaa usimamizi wa JKIA, bunge laambiwa

Twanga pepeta ya Ruto na Raila

adminleo