Habari Mseto

Anayetuhumiwa kumuua Wangechi kushtakiwa mara akipona – Polisi

April 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

TITUS OMINDE na WYCLIFFE KIPSANG

MSHUKIWA wa mauaji ya mwanafunzi wa utabibu katika Chuo Kikuu cha Moi, atashtakiwa kwa mauaji hayo mara tu madaktari wakithibitisha anaweza kujibu mashtaka.

Afisa mkuu wa polisi eneo la Eldoret Mashariki, Bi Lucy Kanani, alisema maafisa wa polisi wanafuatilia kwa karibu jinsi Naftali Kinuthia Njahi anavyopona.

Mshukiwa huyo amelazwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret akitibiwa kutokana na majeraha aliyopata baada ya kujeruhiwa na umati kwa kumuua Ivy Wangechi.

Bi Kanani alisema polisi wanaendelea kuandikisha taarifa kutoka kwa walioshuhudia mauaji hayo karibu na lango la hospitali hiyo mjini Eldoret.

Bi Kanani alisema maafisa ambao wanapeleleza mauaji hayo wataandikisha taarifa kutoka kwa mshukiwa, punde tu baada ya kupata nafuu na kurejesha fahamu.

“Bado hatujaandikisha taarifa kutoka kwa mshukiwa na tunasubiri apate nafuu na kuwa na fahamu, ili aweze kuandikisha taarifa kabla ya kupelekwa kortini,” akasema Bi Kanani.

Afisa huyo alitahadharisha vyombo vya habari pamoja na watumiaji wa mitandao ya kijamii dhidi ya kuendeleza uvumi kuhusu chanzo cha kifo cha marehemu.

“Twaomba vyombo vya habari na watu wanaotumia mitandao watupatie nafasi tukamilishe uchunguzi ili kujua chanzo cha mauaji haya,” akasema.

Wakati huo huo, huzuni imetanda miongoni mwa wanafunzi ambao walikuwa wakisoma pamoja na mwendazake chuoni humo.

Walimtaja Bi Wangechi kama mwanafunzi stadi, ambaye alikuwa gwiji katika masomo yake, mbali na kuwa mchangamfu wa kutangamana vyema na wenzake.

Jana, baadhi ya marafiki wa Wangechi walieleza kuwa mshukiwa alikuwa na mapenzi makubwa kwa marehemu.

Walieleza jinsi Kinuthia alikuwa na mazoea ya kusafiri hadi mjini Eldoret mara kwa mara kutoka Nairobi ili kukutana na Bi Wangechi, lakini mara nyingi hawakuwa wakionana.

Walisema alikuwa akimhepa Kinuthia ili wasipatane, jambo ambalo halikuwa likimfurahisha. Walisema Wangechi mwenyewe aliwaambia alikataa kukutana na mshukiwa katika matukio hayo.

Mshukiwa angefika hadi katika lango la MTRH na kushinda hapo akimsubiri, kisha kuondoka bila kumuona.

Walisema marehemu alikuwa ameanza kujitenga nao bila kuwapa sababu yoyote.