• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Joho ashukuru madiwani kwa kuondolea waziri lawama

Joho ashukuru madiwani kwa kuondolea waziri lawama

Na SAMUEL BAYA

GAVANA wa Mombasa Bw Hassan Joho Jumatano alipongeza bunge kwa kumuondolea lawama waziri wake wa usafiri Bw Taufiq Balala.

Hii ndiyo kauli ya kwanza ya kinara huyo wa kaunti ya Mombasa tangu wiki iliyopita, ambapo bunge la kaunti hiyo lilimuondolea lawama waziri wake.

Kupitia kwa mkurugenzi wa mawasiliano Bw Richard Chacha, Gavana Joho alisema sasa ni muda mwafaka kwa bunge kushirikiana na serikali yake kwa minajili ya kuboresha maendeleo ya wakazi wa Mombasa.

“Ninapongeza bunge kwa kumuondoa lawamani waziri Balala. Hatua hii sasa inatoa mwanya mzuri wa kuendeleza ushirikiano wa kikazi kwa karibu na taasisi hizi mbili muhimu za serikali.

Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba tunaafikia ustawi wa maendeleo ya mwaka wa 2035,” akasema Gavana Joho.

Alisema kuwa sasa kila mmoja likiwemo bunge na serikali yake ana fursa ya kuangalia jinsi ya kuboresha maisha ya wakazi wa Mombasa.

Tamko la Gavana Joho linatarajiwa kupunguza joto la kisiasa ambalo lilikuwa limeanza kujitokeza kati yake na bunge. Bunge limekuwa likihoji utendakazi duni wa mawaziri, jambo ambalo limefanya wakazi wa Mombasa kukosa huduma bora. Hata hivyo, wiki iliyopita baada ya kutathimini ripoti ambayo ilitayarishwa na kamati maalum, bunge liliamua kwamba waziri Balala hakuwa na makosa na kwamba lawama alizolimbikiziwa hazikuwa na msingi wowote.

Mnamo Machi 19, bunge hilo lilipitisha hoja ya kumtimua kazini Bw Balala katika kile ambacho kilitajwa kama utendakazi duni na ufisadi katika wizara yake. Lakini hapo jana Gavana Joho alisema kuwa hatua ya bunge hilo wiki iliyopita ni ishara ya mwanzo mpya ambao lengo lake kamili ni kuhakikisha wakazi wa Mombasa wanapata huduma bora.

“Hii inamaanisha kwamba wakazi wa Mombasa wataendelea kupata huduma bora na kwa ushirikiano wa karibu. Hili ndilo ombi langu,” akasema Gavana. Hata hivyo, kwa mujibu wa Bw Chacha, Bw Joho bado hajapata ripoti ambayo alikuwa akiitarajia kutoka kwa bunge hilo.

Wakati ikitoa ripoti yake bungeni wiki iliyopita, kamati iliyoundwa na spika Arub Khtari ilisema madai yote ambayo yalitolewa bungeni hayakuthibitishwa wakati wa vikao vya umma.

“Kamati maalum ilichunguza madai kadhaa ikiwemo ufisadi, utendakazi duni kinyume na katiba. Pia kwa kuangalia ushahidi ambao waziri Balala alileta katika bunge, ni wazi hakuna ushahidi wa kuunga mkono madai haya.

Kutokana na hilo, basi kamati hii imependekeza kwamba madai yote hayakuwa na ukweli na kwamba hakuna hatua zaidi ambazo waziri Balala anaweza kuchukuliwa,” ikasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kamati hiyo ilieleza bunge kwamba hakuna mkazi wa Mombasa ambaye alijitokeza kutoa maoni yake wakati kamati hiyo ilipokuwa na vikao vya umma kujadilli waziri huyo.

“Ni mwananchi mmoja tu ambaye alitoa madai kadhaa ya ufisadi kuhusu waziri huyo kupitia kwa mtandao wa kijamii. Hata hivyo alionekana kuchanganya mada na hakuweza kuthibitisha hasa alikuwa akilenga hoja ipi dhidi ya waziri,” ikasema ripoti hiyo.

You can share this post!

Sonko ashtakiwa na bwanyenye anayedai kuchafuliwa jina

Raia waandamana kupinga Spika kuteuliwa Rais mpya Algeria

adminleo