Makala

AKILIMALI: Uwekezaji wake katika mizabibu unamlipa vizuri

April 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na SAMMY WAWERU

AGNES Omingo hafichi furaha yake anapozuru kiunga chake cha matunda chenye ukubwa wa karibu ekari tano eneo la Nkoroi, Kaunti ya Kajiado.

Amekipamba kwa matunda ainati, kuanzia karakara, mapapai, matunda yanayoaminika kuongeza damu mwilini -tomarillo, zabibu, matufaha, ndizi na stroberi, haya yakiwa machache tu.

Mizabibu inayozalisha inavutia zaidi, anavuna kadhaa na kumenya.

“Haya ni baadhi ya matunda yenye tija chungu nzima kiafya na kimapato. Hufai kuyakosa shambani, yanastawi popote; maeneo ya baridi kali, kame, na maji mengi. Isitoshe, ni rahisi sana kuyapanda na kutunza,” anafungua jamvi la mazungumzo, akitembeza Akilimali katika kiunga chake.

Licha ya eneo la Kajiado kushuhudia kiangazi mara kwa mara, kaunti hii ina uwezo wa kuzalisha matunda haya. Bi Agnes ameyatengea karibu robo ekari.

Pembezoni ana shimo la maji na kidimbwi, ambapo hutumia jenereta kukuza mizabibu pamoja na matunda mengine.

“Nimefanikisha kulima matunda kwa kutumia mfumo wa mifereji kunyunyizia mimea maji,” anasema mama huyu ambaye pia ni mfugaji wa kupigiwa mfano wa ng’ombe wa maziwa.

Mbolea ya wanyama hao ndiyo huitumia kuendeleza juhudi za kilimo.

Zabibu ni matunda madogo yenye umbo la mviringo na hupatikana kwa rangi mbalimbali hasa kijani, manjano, zambarau, nyeusi na nyekundu.

Mbali na kuliwa, yanatumika kutengeneza jamu, sharubati, jeli, dawa, mvinyo aina ya divai, kukaushwa kuwa zabibu kavu na mbegu zake huzalisha mafuta.

Ni kiini kizuri cha ufumwele (fiber) ambao husaidia katika ukuaji wa viungo vya mwili, hasa kwa mtoto ambaye hajazaliwa. Pia matunda haya yameshamiri Vitamini, bila kusahau madini kama Potassium.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema zabibu ni miongoni mwa matunda yanayosaidia kuzuia magonjwa mbalimbali kama vile Saratani, Moyo, Pumu, shida za kutoona na kusokotwa na tumbo.

Aidha, wanaougua Kisukari wanahimizwa kuyala kwa wingi.

Kumbukumbu za historia zinaeleza kwamba zabibu zilianza kukuzwa Uturuki. Misri, Ugiriki na Roma pia palikuzwa zabibu kwa minajili ya kula na kutengeneza mvinyo.

Ni kufuatia matumizi yake na faida kiafya, ambapo matunda haya yalisambaa Ulaya, Barani Afrika na Marekani.

Misri ni nchi kame, na ni miongoni mwa mataifa bora zaidi duniani katika uzalishaji wa zabibu. Afrika Kusini pia ni mzalishaji mkuu.

Kulingana na Catherine Nyokabi, mtaalamu wa masuala ya kilimo hasa matunda, Kenya haipaswi kuwa na kisingizio chochote kutokuza matunda haya kwa wingi, ikizingatiwa ina mchanga na hali bora ya anga kuyastawisha.

“Hayana kikwazo cha ukame, baridi wala maeneo yenye maji mengi. Hebu angalia Misri, ni kame na ni baadhi ya nchi zinazoyazalisha kwa wingi ulimwenguni. Uturuki nayo baridi ni kali, na inaongoza kwa ukuzaji wa zabibu. Wakulima Kenya ndio sasa wamejua umuhimu wa kuyapanda,” anafafanua, Bi Nyokabi ambaye pia ameyapanda katika Kaunti ya Nyeri na Laikipia.

Asilimia 90 ya zabibu zinazoliwa nchini, huagizwa kutoka nje hasa Misri na Afrika Kusini.

Kiwango cha joto la wastani mchana, kijibaridi usiku na mchanga wenye virutubisho vya kutosha, pamoja na mvua ya kadri maeneo mbalimbali nchini, ni baadhi tu ya vigezo vinavyoiweka Kenya katika ramani ya mataifa yanayoweza kufanikisha kilimo cha zabibu.

Mengi ya matunda haya huzalishwa Meru. Naivasha, Mandera, Kibwezi na Mombasa, pia ni maeneo yaliyotajwa kuwa bora katika kuyalima.

Kuna aina mbili ya matunda haya; yenye mbegu na yasiyo na mbegu (mseto).

Kulingana na wataalamu wa kilimo na wakulima wenye uzoefu wa kuyanda kwa miaka mingi ni kwamba yale mseto ndiyo bora kukuza.

“Ingawa ya mbegu hukua vizuri pia, ya mseto yameibuka kuwa bora zaidi hususan kuzalisha matunda mengi na ya hadhi ya juu,” anaeleza James Macharia, mtaalamu wa zaraa na mkulima wa zabibu eneo la Murang’a.

Taratibu za upanzi

Ni matunda rahisi mno kukuza, ikiwa mkulima ana chanzo cha maji ya kutosha kila wakati. “Kazi huwa kupogoa matawi (prunning), kunyunyizia maji na kuyatunza kwa pembejeo,” anasema Bi Agnes Omingo.

Kitaalamu, shughuli ya kupogoa hupendekezwa ili mmea usalie na matawi yatakayoweza kutunzwa vyema. Ni muhimu kusisitiza kuwa hatua hii hupunguza ushindani wa lishe; maji na mbolea.

Mazao yake hayawi makubwa pekee, ila bora na yenye soko.

Bi Agnes anasema upandaji wa zabibu hauna ugumu wowote ule.

Anapendekeza kuyapanda kwenye mashimo, akishauri urefu wa shimo kuenda chini uwe inchi 12 na upana wa kipimo sawa na hicho.

Bi Nyokabi, mtaalamu wa kilimo, anasema mbali na kipimo hicho, pia yanaweza kuwa na urefu wa futi moja kuenda chini, na upana wa futi moja.

Nafasi kutoka shimo moja hadi lingine iwe kati ya futi 6-8, na laini za mashimo ziwe na nafasi ya futi 10 au mita tatu.

“Wakati wa upanzi, rejesha mchanga wa juu uliochimbwa na kuchanganywa na mbolea, ufikie robo tatu (3/4) ya shimo. Mwagilia maji shimoni, kisha upande ‘mche’ wa mzabibu ambao ni tawi, kwa umakinifu,” ashauri Agnes.

Mtaalamu Nyokabi anahimiza lita tano za maji yamwagiliwe, dakika tano baadaye tawi lipandwe.

Nyasi za boji kuzuia mnyauko wa maji.

Robo ya shimo iliyosalia ni ya kutunza mmea kwa maji na mbolea. Pia, nafasi hiyo hutumika kwa minajili ya kuweka nyasi za boji (mulching), ili kuzuia mnyauko wa maji hasa msimu wa jua kali. Unatakiwa kutumia nyasi zilizokauka kwa sababu hazina wadudu.

“Wakati bora kulisha mizabibu maji ni jioni. Wiki ya tatu hadi nne, matawi yaliyopandwa huanza kuamka,” aeleza Bi Nyokabi, akisisitizia haja ya kuyatunza kwa maji, japo si mengi, na mbolea.

Zabibu huzalishia juu na ndiyo maana hutambaa. Ili kufanikisha shughuli hii, mkulima anashauriwa ‘kupanda’ vikingi kati ya kila mmea. Vinaunganishwa kwa nyaya au kamba dhabiti, ambapo mizabibu husaidiwa kutambaa.

Matunda kuoza

Unaonywa kuwa ukiiruhusu izalishie ardhini, matunda bila shaka yataoza, hivyo basi utakadiria hasara.

“Usisahau kupogoa matawi yanayomea, hasa yale duni, usalie na yale imara ambayo yatakutuza,” aeleza Bi Agnes.

Mazao na mbegu bora

Miezi tisa baada ya upanzi, huanza kuchana maua na kuzaa matunda.

Ekari moja ina uwezo wa kusitiri karibu mizabibu 2,000.

Mavuno ya matunda haya huendelea kwa muda wa miezi mitatu mfululizo, mti mmoja unakadiriwa kuzalisha zaidi ya kilo nne.

Katika maduka ya kuuza matunda na ya kijumla, kilo moja hugharimu zaidi ya Sh400.

Kwa wanaoyanunua shambani kwa minajili ya biashara kama vile kuzalisha mvinyo na kuyauzia maduka, kilo haipungui Sh60.

Mkulima anashauriwa kufanya utafiti wa soko bora kabla ya mavuno, ili kuepuka kero la mawakala.

Ni bayana yanaweza kukuzwa misimu mitatu kwa mwaka nchini.

Kulingana na wataalamu wa kilimo, gharama ya kuyapanda katika ekari moja haizidi Sh100, 000 hii ikidhihirisha wazi wakulima wanaoyakuza kwa wingi wanavuna pesa kama njugu.