• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lugha kama kitambulisho cha makundi ya wanajamii

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lugha kama kitambulisho cha makundi ya wanajamii

Na CHRIS ADUNGO

LUGHA inazidi kutegemewa pakubwa katika jitihada za kuleta mabadiliko na maendeleo kwa wanajamii na huwa na athari chanya na hasi kwa kutegemea watumiaji wake, yaani wasemaji na wasemewa.

Kwa upande wa athari chanya, lugha ni chombo muhimu cha kuwaunganisha watu na kukomesha uhasama miongoni mwa wanajamii.

Hata hivyo, lugha yaweza kuwa na athari hasi hasa ikiwa itatumiwa kuzua fujo au kusababisha utengano kati ya mtu na mtu, jamii na jamii nyingine au hata makundi ya kijamii.

Lugha huweza kuathiri mtazamo na tabia ya mtu. Yote hutegemea namna lugha itakavyotumiwa ili kuleta athari inayokusudiwa.

Watu hutambua kikundi chao cha kijamii kwa kutegemea misimbo au aina ya lugha wanayoitumia.

Matumizi ya lugha kwa njia fulani ndiyo huwafungamanisha watu wa kikundi fulani pamoja na kuwatambulisha. Lugha ya maafisa wa polisi kwa mfano, ina uwezo wa kuwatambulisha.

Maafisa wa polisi ndio kiungo muhimu katika kulinda na kudumisha usalama wa nchi.

Kutokana na kazi yao, wao huhusiana na watu wa matabaka mbalimbali na walio na vyeo tofauti tofauti katika nyanja mbalimbali.

Wao hutumia lugha kwa namna inayowatambulisha wao kama kikundi maalumu ambacho kinaweza kutambuliwa kutokana na sajili yao.

Kikundi hiki cha maafisa wa polisi kinaweza kutambuliwa na watu wengine kutokana na lugha wanayoitumia.

Kama wasemavyo Linda na Wareing (1999:143), kikundi fulani hutambuliwa kama kikundi cha kijamii na watu wengine kutokana na upekee wa matumizi yao ya lugha na tabia nyingine za kiisimu kama vile namna wanavyotunga sentensi zao.

Haya ndiyo mambo ambayo huwaongoza wanajamii wengine kukitambua kikundi cha kijamii.

Matumizi ya lugha ya maafisa wa polisi kwa mfano ni ya kipekee na hii huwatofautisha na makundi mengine ya watu katika jamii.

Mitindo

Lugha ni chombo muhimu cha mawasiliano katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali. Habwe na wengine (2010:71) wanasema kuwa “… ili kukidhi haja ya mawasiliano, makundi ya kijamii huibua mitindo na istilahi zao zinazowawezesha kurejelea shughuli za kundi husika.”

Hii inaashiria kuwa kila kikundi katika nyanja mbalimbali huwa na mtindo wake wa kutumia lugha kwa namna ambavyo itawawezesha kuafikia malengo yao ya kazi.

Maafisa wa polisi kama kikundi cha kijamii pia huwa na mitindo na istilahi zao ambazo huwawezesha kutekeleza majukumu yao.

Kwa mujibu wa Fishman (1968:3), jamii ni ya muhimu kuliko lugha na kwa hivyo anasema kuwa jamii ndio hutuwezesha kupata muktadha ambao unaweza kutusaidia katika kutazama aina ya lugha inayotumiwa.

Kama asemavyo Bernstein (1971:61), tofauti za kiisimu za matumizi ya lugha ya kikundi fulani hutokea katika mazingira halisi ya kijamii na vyeo vya makundi mbalimbali huweza kubainishwa na usemi wao.

Ni rahisi kuchunguza sajili ya maafisa wa polisi wanapokuwa katika kituo cha polisi kwa kuwa hayo ndiyo mazingira yanayowatambulisha na ndiyo muktadha wao halisi.

Fishman (1968:139) akimnukuu Halliday, anasema uchunguzi wa muktadha wa mazungumzo hutuelekeza katika uchanganuzi wa hali na matumizi ya lugha.

Pride (1971:25), anasema kuwa mawanda ya matumizi ya lugha huelezwa kama hali ambapo matumizi ya aina fulani ya lugha hutumiwa na kikundi mahsusi na hii husaidia katika utambulisho wa kikundi hicho cha kiisimu na kwa njia ya kijamii.

Hii inaashiria kwamba kikundi fulani cha watu huweza kuainishwa kijamii na kiisimu.

Namna watu hutumia lugha husababishwa na mambo mawili: wao kama watu binafsi au wao kama wanajamii.

Hii ina maana kuwa, lugha wanayotumia katika mazungumzo huchangia katika kujitambua na pia lugha yao ni chombo cha kudhihirisha kikundi hicho husika.

Miundo

Kutokana na maelezo ya wataalamu hawa, ni wazi kuwa kila kikundi katika nyanja mbalimbali huwa na namna yao ya kuwasiliana. Hii huwatambulisha watu wa kikundi hicho.

Muundo wa kitabaka huathiri elimu na kazi za watu na kisha kuwapa wanajamii husika mahusiano fulani ambayo hutambulisha tabaka lao ambalo huwa tofauti na matabaka mengine.

Wanajamii katika kikundi fulani hutumia lugha kwa njia ya kipekee wanapoingiliana ili kutambuliwa katika kikundi hicho. Hii inadhihirisha kwamba unaweza kuzungumza kama wanakikundi hicho na hivyo kuwa mwanakikundi.

Nchini Kenya kwa mfano, kuna chukulizi kuwa lugha ya maafisa wa polisi husheheni kuchanganya ndimi, sauti yao hudhihirisha mamlaka na wana misimbo yao ambayo hutumiwa katika mawasiliano miongoni mwao.

Misimbo

Msimbo ni sehemu ya lugha na ni utaratibu wa kutoa mawasiliano (Iribemwangi na Mukhwana, 2011:45).

Wanaendelea kusema kwamba kwenye msimbo finyu, wazungumzaji huweza kutumia ujuzi na tajriba zao za pamoja na uelewa wa pamoja kusemea kile wanachotaka kuongea au kusema.

Aina hii ya msimbo huunda upamoja ambao hufanya watu wanaotumia lugha kuhisi kuwa wao ni wa kundi fulani.

Kama mkakati wa mawasiliano, baadhi ya watu hasa maafisa wa usalama hutumia msimbo finyu kama njia ya kuonyesha umoja na kutenga makundi mengine hasa wanapozungumzia masuala yanayohusu usalama wa nchi.

Pia hutumia msimbo pana wanapowasiliana na wateja wao.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nilidhani baada ya mke kumuacha angenioa...

Kocha matumaini Shujaa watang’aa Singapore Sevens

adminleo