Kalonzo sasa ni wakili wa Gavana Ngilu
Na CECIL ODONGO
Kwa ufupi:
- Bw Kalonzo na mawakili wengine walipinga hatua ya NCIC kumsomea gavana huyo wa chama cha NARC madai tofauti
- Alisema mteja wake anaandamwa na wanasiasa wakuu wanaopinga juhudi zake za kulinda mazingira kaunti ya Kitui
- Kiongozi huyo alimtaka Bi Ngilu asimame imara kuhusiana na utekelezaji wa marufuku dhidi ya usafirishaji makaa na uzoaji wa mchanga
- Gavana wa Kiambu Bw Ferdinard Waititu pia aliingilia suala hilo na kutaka Bi Ngilu akabiliwe kisheria
KINARA wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka Jumatatu alijikumbusha taaluma yake ya uwakili, alipoandamana na gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu katika afisi za Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) akiwa wakili wake mkuu.
Makamu huyo wa rais wa zamani alijitokeza mbele ya tume hiyo inayoongozwa na Bw Francis Ole Kaparo, akiwa wakili mkuu wa Bi Ngilu.
Bi Ngilu alikuwa ameitwa kuhusiana na madai ya kuchochea uchomaji wa lori la kampuni ya usafiri ya Juja Transporters.
Hata hivyo, Bw Kalonzo na mawakili wengine walipinga hatua ya NCIC kumsomea gavana huyo wa chama cha NARC madai tofauti.
Bi Ngilu akiwa ameandamana na kundi la akina mama waliomsifu kwa nyimbo, alijulishwa kuwa alitoa matamshi ya uchochezi.
Mawakili wake walipinga hatua hiyo mpya, na kusema kuwa tume hiyo ilikuwa na njama fiche. Kwa hivyo walimshauri Bi Ngilu kuitikia wala kuzungumza chochote hadi NCIC itoe maagizo mapya.
Vita vya kisiasa
Akiwahutubia wanahabari, Bw Kalonzo alisema mteja wake anaandamwa na wanasiasa wakuu wanaopinga juhudi zake za kulinda mazingira kaunti ya Kitui.
“NCIC wametupotezea wakati kwa sababu hata hawajawasilisha madai tuliyoyatarajia. Vita dhidi ya Gavana Ngilu ni vya kisiasa na wanaotaka ukame uwe janga la kitaifa,” akasema Bw Kalonzo.
Japo Bi Ngilu hakuzungumza na wanahabari, Bw Kalonzo alimtaka asimame imara kuhusiana na utekelezaji wa marufuku dhidi ya usafirishaji makaa na uzoaji wa mchanga kwenye kaunti yake.
Mawakili wengine waliofika kumtetea Bi Ngilu ni Bw Martin Oloo, Bw Daniel Maanzo, Davison Makau na Bi Rachel Osendo.
Wabunge wengine wa chama cha Wiper na mwaniaji wa ugavana kaunti ya Machakos Wavinya Ndeti waliandamana na Gavana Ngilu katika makao makuu ya tume hiyo.
Kuchoma lori
Bi Ngilu alikuwa anakabiliwa na madai ya kuchochea kundi la vijana kuchoma lori la mfanyibiashara mmoja kutoka kaunti Kiambu, lililokuwa likisafirisha makaa.
Wiki iliyopita, mwanasiasa huyo ambaye amewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali za uwaziri serikalini, alifika katika makao makuu ya idara ya upelekezi wa Jinai (DCI ) na kuandikisha taarifa kuhusiana na tukio hilo.
Kuchomwa kwa lori hilo kulizua maandamano mjini Limuru, waandamanaji wakimlaumu gavana huyo kwa kuendeleza ukabila.
Gavana wa Kiambu Bw Ferdinard Waititu pia aliingilia suala hilo na kutaka Bi Ngilu akabiliwe kisheria.
Awali, Bw Waititu aliongoza wanasiasa wengine wa eneo la Kati kutaka hatua za haraka zichukuliwe, ili kumdhibiti Bi Ngilu.