• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Jinsi makaa spesheli yanavyosaidia kupunguza gharama ya upishi

Jinsi makaa spesheli yanavyosaidia kupunguza gharama ya upishi

NA SAMMY WAWERU

GHARAMA ya maisha na uchumi inazidi kuwa ghali kila uchao, kuanzia bidhaa za kula, vifaa vya mapishi, usafiri kuelekea kazini na uchukuzi.

Licha ya mfumko huo, kiwango cha mapato kimesalia kilipokuwa awali.

Bei ya mafuta ya petroli nchini imeandikisha ongezeko la juu zaidi, sawa na ile ya gesi ya kupikia.

Watu sharti wale, liwe liwalo.

Huku wananchi wakiendelea kulemewa na bei ghali ya gesi, John Mwangangi anafanya awezalo kuwaletea afueni.

Akiwa mwalimu mstaafu aliyekuwa akifunza Somo la Kiswahili katika Kaunti ya Nyeri, Mwangangi aliingilia biashara ya utengenezaji makaa kwa njia ya Kisayansi, kabla kuweka chaki chini.

Maarufu kama briquettes, ni makaa yanayoundwa kwa kutumia malighafi yanayopatikana kwa wingi mashinani, muradi yawe yanayoweza kuchomeka kuwa jivu yakiwa yamekauka.

Malighafi hayo ni; majani yaliyokauka, unga unaotokana na upasuaji wa mbao (sawdust), mabaki ya makaa ya kuchomwa, jivu, na pia karatasi.

Utengenezaji wa briquettes, Mwalimu Mwangangi hajauanza hii leo, jana wala juzi.

Anasema, safari yake katika makaa hayo iling’oa nanga hata kabla ya Kenya kutangaza kuanza kutekeleza marufuku ya ukataji miti na uharibifu wa misitu ya serikali 2018.

“Amri hiyo ilipoanza kutekelezwa, ilitia muhuri wazo langu kusaidia kudumisha usalama wa miti na misitu yetu,” asema.

Ukataji wa miti kiholela kwa minajili ya makaa, unatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya hali ya anga na tabianchi.

Kuanzia kiangazi na ukame unaoendelea kushuhudiwa katika kaunti 23, ongezeko la kiwango cha joto, yote hayo yanahusishwa na uharibifu wa miti na misitu.

Kulingana na ripoti ya majuzi ya Shirika la Chakula na Kilimo, FAO – UN, Kenya ni miongoni mwa nchi tatu zilizolemewa na makali ya kiangazi Upembe wa Afrika.

Orodha ya mataifa hayo pia inajumuisha Somalia na Ethiopia.

Hatua ya Mwangangi kuingilia utengenezaji wa briquettes, anasema ni ya busara hasa katika kusaidia kunusuru maliasili ambayo ni kivutio cha mvua.

Katika boma lake, eneo la Gathugu, Karatina, Kaunti ya Nyeri, ana karakana mbili ya shughuli hiyo.

Moja, ni ‘kiwanda’ cha kutengeza umbo sampuli ya briquettes, baada ya malighafi kuchommwa na kuchanganywa na maji.

Ana mashine inayounda vipande hivyo.

John Mwangangi akionyesha jinsi mashine inavyotumika kutengeneza makaa hayo spesheli. PICHA | SAMMY WAWERU

Kulingana na Wanjiru Kuria, mjasirimali mwenye uzoefu wa miaka mitano katika makaa hayo spesheli, mashine hiyo inagharimu Sh145, 000.

“Nilisaidiwa na wazazi wangu kuinunua, nilipoingilia utengenezaji wa briquettes,” aelezea mfanyabiashara huyo, ambaye kwa sasa anaridhia biashara ya makaa hayo.

Karakana ya pili ya Mwangangi, ni ya kuyakausha yanapotoka ‘kiwandani’.

Juu na kandokando, imeezekwa kwa karatasi ngumu ya nailoni kiwango cha joto ndani kikiwa cha juu sawa na kichashuhudia katika kilimo cha mvungulio.

“Meza unazoona humu, ni za kuyakausha kulingana na yalivyotengenezwa,” asema.

Ili briquettes zikauke sambamba, Mwangangi anasema hutegemea msimu.

“Msimu wa mvua au mawingu yakitanda, huchukua muda mrefu kukauka.”

Malighafi huchomwa, yanakuwa jivu kisha yanachanganywa na maji.

Yanapitishwa katika mashine spesheli, yenye vifaa vya umbo wa makaa ya briquettes.

“Yakishakauka, yanakuwa tayari kuingia sokoni,” Mwangangi aelezea.

Wananchi wakiendelea kulalamikia gharama ya juu ya gesi, Mwangangi huuza mkebe wa kilo mbili Sh100.

Isitoshe, matumizi ya briquettes ni nafuu ikizingatiwa kuwa moto wake unadumu muda mrefu.

Wateja wake, ni wenyeji wa Karatina na viunga vyake.

Akiridhia ukakamavu na mchango wake kusaidia kupunguza gharama ya upishi, Mwalimu Mwangangi anasisitiza ni jukumu la kila Mkenya kujituma kuokoa na kudumisha usalama wa mazingira.

“Endapo una uvumbuzi utakaosaidia kunusuru mazingira, usisite kuutekeleza. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinagusa kila mmoja wetu,” ashauri.

  • Tags

You can share this post!

Kamati ya kufuatilia shughuli za uchaguzi Pwani yazinduliwa

Kampeni: IEBC yapendekeza Ruto na Raila wachunguzwe

T L