• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Ronaldo ala sifa kuokoa Juventus dhidi ya Ajax dimbani

Ronaldo ala sifa kuokoa Juventus dhidi ya Ajax dimbani

Na MASHIRIKA

AMSTERDAM, Uholanzi

KOCHA wa Juventus, Massimiliano Allegri alimmiminia sifa tele mvamizi nyota Cristiano Ronaldo akimtaja kuwa katika kiwango tofauti na wengine baada ya kupachika bao muhimu la ugenini katika sare ya 1-1 dhidi ya wenyeji Ajax kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Jumatano.

Ronaldo, ambaye alikuwa anarejea kutoka mkekani, aliweka Juventus kifua mbele sekunde chache kipindi cha kwanza kitamatike kwa kufuma kichwa kisafi na kuimarisha rekodi yake ya mabao katika mashindano haya hadi 125.

Uongozi huu haukudumu kwani Ajax ilisawazisha kupitia winga Mbrazil David Neres mara tu kipindi cha pili kilipoanza.

“Ronaldo alionyesha kwamba yuko katika kiwango tofauti. Uamuzi wake na juhudi zake ni tofauti na mchezaji mwingine yeyote, na hakuna unachoweza kufanya,” Allegri alisema.

“Yeye ni mchezaji ambaye ana ujuzi wa kipekee kuliko wengine.”

Ajax iliongeza presha uwanjani Johan Cruyff, ikikosa bao mara kadhaa kabla ya Douglas Costa kukaribia zaidi kuzamisha chombo cha Juve dakika za lala salama wakati shuti lake lilipogonga mwamba.

Cristiano Ronaldo (kushoto) wa Juventus awania mpira dhidi ya beki Daley Blind wa Ajax mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya Aprili 10, 2019, uwanjani  Johan Cruijff ArenA jijini Amsterdam. Picha/ AFP

Ufufuo wa Ajax katika mechi iliyopita dhidi ya Real Madrid ilipofuta kichapo cha mabao 2-1 ilichopata nchini Uholanzi kwa kucharaza Wahispania hao 4-1 uwanjani Santiago Bernabeu ni ishara kuwa mchuano huu bado ni mbichi.

“Ni matokeo mazuri kwa sababu tulipata goli la ugenini, mechi bado ni wazi,” aliongeza Allegri, ambaye analenga kuongoza Juventus kushinda soka ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996 walipokanyaga Ajax mjini Roma.

“Tulikuwa wazuri katika kulinda ngome yetu, timu ilikuwa nzuri na yenye mshikamano, kuna sababu nzuri ya kuwa na matumaini tunaweza kutinga nusu-fainali.

“Hatuna wasiwasi, tunaheshimu Ajax sana, lakini lazima tuwe tayari. Sare ya 1-1 ni bora kuliko 0-0, mjini Turin tutahitaji kutafuta ushindi.”

Zaidi ya mashabiki 140, wengi wao wa Juventus, walikamatwa wakimiliki silaha hatari kabla ya mchuano huu, polisi nchini Uholanzi walisema.

Vikundi viwili tofauti vilisimamishwa na polisi, huku mashabiki 46 wakizuiliwa katika kituo cha polisi kabla ya wengine 61 kukatazwa kuingia ugani Johan Cruyff.

Zaidi ya mashabiki 30 kutoka Uholanzi pia walikamatwa katika lango la mashabiki wa nyumbani wakiwasha fataki, kurusha mawe na kuvunja madirisha.

You can share this post!

Wakazi wa Ruiru wahimizwa kuzingatia lishe bora ili...

Harambee Stars roho mkononi droo ya Afcon ikitangazwa Cairo

adminleo