Magaidi walivyoteka madaktari wa Cuba katika kaunti ya Mandera
WATU wanaoaminika kuwa magaidi wa Al-Shabaab mnamo Ijumaa walivamia na kuteka nyara madaktari kutoka Cuba wanaohudumu katika kaunti ya Mandera.
Madaktari hao walikuwa wakielekea kazini wakitumia gari la serikali ya kaunti hiyo saa tatu asubuhi, huku wakiwa wamelindwa na maafisa wawili wa polisi, walipovamiwa barabarani, eneo la Banisa.
Walioshuhudia uvamizi huo walisema, baada ya kuzuia gari lililokuwa likisafirisha maafisa hao magaidi hao walianza kuwafyatulia risasi polisi, ambapo walimuua afisa wa AP, Hussein Katambo Ngala.
Afisa mwenzake kutoka idara ya polisi wa kawaida alifanikiwa kutoroka.
Wavamizi hao baadaye waliwashurutisha madaktari hao kuingia katika gari lao, kisha wakaondoka haraka.
“Walizuiwa na magari mawili aina ya Toyota Probox njiani. Kwa bahati mbaya, afisa wetu wa AP alipigwa risasi na akafariki papo hapo,” akasema msemaji wa polisi Charles Owino. Baadaye magaidi hao walivuka mpakani kuelekea Somalia,” Bw Owino aliongeza polisi sasa wanamzuilia dereva aliyekuwa akiwasafirisha madaktari na maafisa hao, kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
“Maafisa wetu wote wa usalama hadi wa jeshi wamekuja pamoja na wanaendelea kufuata hao magaidi katika mpaka wetu wa Kenya na Somalia,” akasema Bw Owino.
Japo polisi hawakutaja madaktari waliotekwa nyara, kulingana na habari kutoka kwa wizara ya afya, daktari wa upasuaji Landy Rodriguez na Dkt Assel Herera Correa ndio walitumwa katika kaunti hiyo, ambayo inapakana na Somalia.
Polisi waliokuwa wamewafuata wavamizi hao walirejea na habari za kutamausha kuwa hawakujua njia ambayo magari yao yalitumia, wakisema operesheni ya kuwasaka ilikuwa imepokezwa kwa wanajeshi.
“Maafisa wetu walipata barabara tatu baada ya kuingia Somalia na hawangejua ile wavamizi walitumia,” akasema afisa wa polisi.
Bado hali ya madaktari hao haikuwa imejulikana kufikia Ijumaa.