• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
MWANAMUME KAMILI: Ukipendwa pendeka, nayo macho ya pembeni yazibe!

MWANAMUME KAMILI: Ukipendwa pendeka, nayo macho ya pembeni yazibe!

Na CHARLES OBENE

KILA mara tunashuhudia vita vya nyumbani baina ya watu ambao ni muhali kuzozana!

Si ajabu kwamba wachumba wa leo wanafarakana na hata pete za uchumba kutumbukizwa pangoni ama kubondwabondwa kwa nyundo!

Mwanadada mmoja alivua pete ya thamani kubwa na kuitumbukiza kilindini mwa mto. Kisa na maana? Kutoaminiana!

Ajabu ni kwamba kidosho yule na mumewe walikuwa tayari wamekwisha ahidiana kufa kuzikana na walikuwa katika pilkapilka za harusi.

Lakini jambo moja liliwasumbua moyoni. Shaka na shauku! Walitiliana shaka kubwa licha ya kwamba walikuwa tayari wamefunga nyoyo zao pamoja. Iweje shaka kushamiri ndani ya upendo?

Nini hasa kilichogusa mkia wa nyoka na kutibua mambo?

Nilidokezewa kwamba mwanamke hakufurahia tabia za mumewe kila mara kuondoka nje kupokea simu zilizopigwa usiku.

Isitoshe, alitilia shaka mienendo ya mumewe hasa tabia za kupigiwa simu nyakati za usiku. Ole nyinyi mnaothamini mno usuhuba kuliko muamana wa familia!

Kuna baadhi ya wanaume kwa wanawake wa leo wasiojua adabu wala heshima kwa mwenza.

Yaani unawapa kila kitu! Si nafsi si moyo lakini bado hawaridhiki! Umekwisha kuwapa vyote vya kupewa mtu lakini bado wanataka usuhuba pembeni.

Ipi mipaka?

Raha yao kulimbikiza himaya ya marafiki wasiojua mipaka ya mzaha.

Jamani mnataka nini duniani nyie wenye tabia hizi duni? Mwanamume kamili sharti kujua mwisho wa mzaha.

Mara kwa mara ninaona tabia za wanaume kuficha simu zao usiku ama wengine wanazima kabisa!

Wengine nao wanaona heri simu kulazwa kifudifudi, uso na mwanga wake usionekane!

Sijui na sitaki kujua sababu ya tabia hizi za baadhi ya wanaume wa leo. Nijuavyo ni kwamba siku za mwizi ni arobaine.

Hakuna mke akijua thamani yake vyema atavumilia usumbufu wa nje mara kwa mara. Usiku wa manane simu kukiriza ni ishara ya nyumba isiyokwisha dhiki. Ni ishara ya mchezo wa paka na panya tu.

Nyumba na chumba haishi adabu na heshima. Sharti mume na mke kukomaa na kujua ukweli huu.

Wekeni mipaka ya mzaha nyie mnaotaka ushuba na dunia nzima! Mtu kukupa moyo na nafsi yake nawe usione heri kumpa japo heshima?

Kwa uchimvi huu mtasalia na hadithi za paukwa pakawa miaka na mikaka! Nani mwenye kulaumiwa kwa kosa la uongo kushamiri katika uhusiano au hata nyumbani baina ya mke na mume?

Nazo ndimi zenu zinanena nini kuhusu uhalisi wa mambo ambayo si dhahiri kwa jicho la pembeni?

Hekima ya uwazi ina msingi kwamba wanadamu wanastahili kuyaweka wazi ya wazi hata kama yanaweza kumtoa mtu roho. Hii ni kwa sababu wanyonge huanza safari kwa subira na uvumilivu.

Heshima ndio shina kuu la upendo nyumbani. Huo ndio ungwana wa mwanamume kamili.

[email protected]

You can share this post!

SHERIA: Wahitaji idhini ya mkeo kushiriki naye tendo la ndoa

UMBEA: Dalili tosha za mwanamume atakayekufanya uchukie ndoa

adminleo