• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
JAMVI: Je, Raila alijichimbia kaburi kukubali handisheki ya Uhuru?

JAMVI: Je, Raila alijichimbia kaburi kukubali handisheki ya Uhuru?

NA CECIL ODONGO

KIONGOZI wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga amejipata katika njiapanda kisiasa baada ya baadhi ya washirika wake na wafuasi kumtaka ajiondoe kwenye muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Ingawa Bw Odinga amekuwa mwanasiasa mzoefu ambaye amekuwa akipenyeza njia zake na kuibuka mahiri kwenye mtanziko wa kisiasa, madai kwamba Rais Uhuru Kenyatta anatumia ushirikiano huo maarufu kama ‘handsheki’ kumchimbia kaburi la kisiasa linaendelea kushamiri.

Kiini cha wafuasi na washirika wa Bw Odinga kumtaka ajiondoe kwenye ndoa yake ya kisiasa na Rais ni kuendelea kufifia kwa umaarufu wa chama chake cha ODM na pia makubaliano hayo kumfunga kisiasa huku mpinzani wake mkuu, Naibu Rais Dkt William Ruto akiendelea kujiandaa kwa uchaguzi wa 2022 kwa kujinadi kwa wapigakura maeneo mbalimbali ya nchi.

Hatua ya Bw Odinga kujiepusha na siasa za 2022 na kutotangaza wazi msimamo wake kuhusu uwaniaji wa wadhifa wa Urais imewaacha wafuasi wake wengi kwenye njia panda huku wachanganuzi wa kisiasa wakidai Dkt Ruto anatumia mwanya huo kujizolea umaarufu katika ngome za Bw Odinga.

Kuonyesha kwamba hali si hali kwa kinara huyo wa upinzani, mshirika wake wa karibu ambaye pia ni kakake mkubwa Dkt Oburu Oginga kwenye mahojiano na gazeti moja nchini, alieleza wazi kuwa Bw Odinga hafai kuendelea kushirikiana na Rais Kenyatta iwapo kasi ya vita dhidi ya ufisadi itaendelea kupungua jinsi ilivyo kwa sasa.

Matamshi ya Dkt Oginga ambaye pia ni mbunge mteule kwenye Bunge la Afrika ya Mashariki (EAC), yalitokana na kauli ya Rais Kenyatta wakati akihutubia taifa bungeni wiki jana kwamba vita dhidi ya ufisadi vitaendeshwa kulingana na sheria na si kupitia kupiga siasa kwenye mikutano ya hadhara.

Kauli hiyo ilionekana kuwakera viongozi wa ODM ambao wamekuwa wakishinikiza mawaziri na maafisa wa serikali waliotajwa kwenye visa vya ufisadi wajiuzulu, baadhi wakimhusisha Dkt Ruto na uovu huo.

Kulingana na Dkt Oginga, Bw Odinga amekuwa na sifa ya kupigiwa mfano kwenye jitihada za kumaliza ufisadi na hafai kushirikiana na serikali ambayo haionekani kumakinikia vita vya kuangamiza dondasugu hilo nchini.

“Vita dhidi ya ufisadi vinafaa kuzidishwa na iwapo kuna dalili zozote za ulegevu basi sidhani kama Bw Odinga atafurahi kuendelea na ushirikiano huu. Suala hili ndilo lilikuwa msingi wa mariadhiano kati ya Rais na Bw Odinga.

“Hata hivyo, sijui iwapo ametafakari kujiondoa.Sijashauriana naye kuhusu hilo lakini kwa kuwa yeye ndiye alihusika kwenye ‘handsheki’, uamuzi wa kujiondoa ama kutojiondoa ni wake,” akasema Dkt Oginga.

Kulingana na mchanganuzi wa kisiasa Martin Andati, kauli ya Dkt Oginga ambaye amekuwa mwelekezi wa kisiasa wa nduguye tangu kifo cha baba yao Jaramogi Oginga Odinga Januari 1994, inaashiria kwamba joto la kisiasa linazidi kupanda kwa kigogo huyo wa siasa za upinzani baada ya kugundua matarajio yake hayakutimizwa kwenye ‘handsheki’.

“Ukisikia Dkt Oburu anazungumza unafaa kujua hiyo ni sauti ya Bw Odinga na ni ishara kuwa kiongozi huyo wa ODM amegundua alichezewa shere na Rais.

“Kinara huyo wa upinzani mara nyingi hutumia nduguye kupima kina cha maji kwenye mawanda ya kisiasa na sasa ni dhahiri kwamba anatafakari upya kuhusu uhusiano wake na Rais. Yaelekea amegundua kwamba anapoteza sana. Pengine alikuwa na matarajio kwamba wandani wake wangeteuliwa mawaziri au katika nyadhifa nyingine na hilo halijatimia hadi sasa,” akasema Bw Andati.

Msomi huyo hata hivyo anasema matumaini ya pekee ya Bw Odinga ni kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kisha Naibu Rais adhibitiwe kisiasa lakini hilo pia huenda likakosa kutimia ikizingatiwa muda uliosalia kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2022 ni mfupi mno.

“Tumaini la pekee la Bw Odinga ikiwa atasalia kwenye ‘handsheki’ ni kufanyika kwa kura ya maoni ingawa kwa mtazamo wangu hilo litakosa kutimia baada ya muda wa kamati ya kujenga madaraja (BBI) kuongezwa hadi mwezi Oktoba mwaka huu,”

“Hata hivyo kuendelea kwa Bw Odinga kushirikiana na serikali kunaumiza wafuasi wake ambao sasa hawana mwelekeo na kurahisisha kazi ya wapinzani wake kuwatupia chambo. Wafuasi wengi wanaendelea kuchukizwa na hatua ya kiongozi wao kuendelea kutilia manani ushirikiano na Rais ilhali Bw Ruto yupo kiguu na njia akilenga 2022,” akaongeza Bw Andati.

Jumapili iliyopita baada ya mechi ya soka kati ya Gor Mahia na RS Berkane ya Morocco uwanjani Kasarani, mashabiki walimkabili Bw Odinga na kumweleza peupe kwamba hawakufurahisha na kushindwa kwa chama cha ODM maeneobunge ya Ugenya na Embakasi Kusini.

“Toka kwenye hiyo handshake na ujitayarishe kwa 2022. Hatutakubali uendelee kuwa serikalini na Ruto anacheza siasa… hiyo handshake haitusaidii. Hatuwezi kushindwa Embakasi Kusini, Ugenya na Kasarani,” wakasema mashabiki wenye hasira waliojaribu kumtia adabu Gavana wa Siaya Cornel Rasanga na kuwalazimisha walinzi kuingilia kati.

Mashabiki hao walidai hatua ya Bw Odinga kutomfanyia mgombeaji wa ODM Chris Karan kampeni na Bw Rasanga kuwatishia wakazi wa Ugenya kuwa hawatapokea miradi ya maendeleo, ndizo zilichangia ODM kushindwa kwenye uchaguzi huo mdogo.

Hata hivyo, mbunge wa Westlands Timothy Wanyonyi kupitia mahojiano na Jamvi alisema kwamba ni mkondo wa mambo kwenye serikali ya Jubilee ndio utaamua iwapo Bw Odinga ataondoka serikalini au la.

“Nafikiri wanaolalamika wamesahau Bw Odinga ni nani kwenye siasa za taifa hili. Leo akiamua kuondoka kwenye handsheki, hali itakuwa vingine na huenda tukakosa umoja na utulivu unaoshuhudiwa kwa sasa,” akadai Wanyonyi.

“Chaguzi ndogo za Embakasi Kusini na Ugenya hazifai kutumika kudhihirisha kuwa siasa za Bw Odinga zinaendelea kufifia na umaarufu wa ODM unapotea. Ingawa hivyo naunga mkono wazo la Dkt Oburu kwamba iwapo mambo hayaendi kwa msingi ulioanzisha ‘handsheki’ basi kiongozi wangu wa chama hana sababu ya kuendelea kushirikiana na Rais Kenyatta,” akasema Bw Wanyonyi.

Mbunge huyo hata hivyo anasema mustakabali wa kisiasa wa kinara huyo wa chama cha ODM unategemea mapendekezo ya BBI na kuandaliwa kwa kura ya maamuzi wakati au kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2022.

You can share this post!

TOM MBOYA: Mtetezi wa haki za wafanyakazi nchini na...

Sababu za Raila kukosa udhibiti wa kisiasa Luo Nyanza

adminleo