• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wazazi wa waliotekwa nyara wadai kuandamwa na ushetani

Wazazi wa waliotekwa nyara wadai kuandamwa na ushetani

Na MASHIRIKA

WAZAZI wa wasichana waliotekwa nyara Chibok, wanahofia kuandamwa na nguvu za kishetani miaka mitano tangu kisa hicho kilipotokea watoto wao walipokuwa shuleni, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Miongoni mwa wasichana zaidi ya 200 ambao walitekwa nyara katika mabweni yao mnamo Aprili 14, 2014, ni wasichana 107 pekee ambao wamepatikana kufikia sasa kufuatia makubaliano kati ya serikali na kundi la kigaidi la Boko Haram lililohusika.

Yakubu Njeki, ambaye ndiye Mwenyekiti wa chama cha wazazi wa wasichana waliotekwa nyara, alisema wanapitia masaibu mengi, ambayo yamewafanya kuamini kuna nguvu za giza zinazowaandama.

Alitoa mfano wa kisa kilichotokea Aprili mwaka uliopita wakati wazazi wa baadhi ya wasichana walioachiliwa huru, walipohusika kwa ajali mbaya barabarani , iliyosababisha mmoja kufariki na wengine 17 kujeruhiwa.

Walikuwa wakienda mkutanoni katika Chuo Kikuu cha Yola ambako watoto wao wanapokea mafunzo maalumu yaliyofadhiliwa na serikali.

Januari mwaka huu, ndugu na dada za baadhi ya wasichana ambao hawajapatikana, walikuwa wakirudi shuleni ambapo wanafadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali, wakati gari walimokuwa wakisafiria lilipopata ajali.

Wanane kati yao walijeruhiwa vibaya, pamoja na katibu wa chama hicho cha wazazi, Zannah Lawan aliyekuwa akiwapeleka shuleni.

Wiki kadhaa baadaye, mnamo Machi baada ya watoto waliojeruhiwa kupata nafuu, walikuwa wakirejea shuleni walipopata ajali tena. Wakati huu, Nkeki ndiye alikuwa nao.

“Kuna kitu kinatuandama kwa njia moja au nyingine. Gari lilibingiria lakini sikujeruhiwa. Mambo haya yanayofanyika si ya kawaida,” akasema.

Kwa jumla, wazazi 34 wa watoto waliotekwa nyara wamefariki tangu wakati huo hadi sasa kwa sababu mbalimbali ikiwemo ajali, maradhi na hata mashambulio ya Boko haram.

“Siki hizi sipendi kuwaalika wote mkutanoni. Huwa nachagua watu wachache watakaosikiliza vyema kisha wapeleke ujumbe kwa wengine,” akaeleza Nkeki.

Mapema mwezi huu, wawakilishi wa chama hicho cha wazazi walisafiri zaidi ya saa 48 kutoka Chibok hadi Lagos kukutana na mhubiri mashuhuri TB Joshua.

“Hakuna habari zozote tunazopokea kuhusu wasichana ambao bado wako mwituni. Hakuna mtu anayekuja kutuambia chochote kuhusu wasichana hao ndiposa tuliamua kupeleka jambo hili kwa Maulana,” akasema mmoja wa wazazi, Yana Galang.

Garba Shehu, ambaye ni msemaji wa Rais Muhammadu Buhari, alisema juhudi bado zinaendelezwa ili wasichana wote warudishwe nyumbani.

Aliongeza kuwa hali hiyo imekumbwa na changamoto kwa sababu Boko Haram iligawanyika na kuna upande mmoja usiotaka kulegeza misimamo yake.

You can share this post!

Mlima Kenya utahama Jubilee – Moses Kuria

ONGAJI: Karaha kwenye barabara kuu ya Thika zitatuliwe

adminleo