155 waliobobea katika KCSE 2018 kusomea udaktari
Na WANDERI KAMAU
IDADI kubwa ya waliong’aa kwenye mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) 2018 watasomea udaktari, kulingana na ripoti ya mpangilio wa kuwaita kwa vyuo vikuu iliyotolewa jana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha.
Kulingana na ripoti hiyo, wanafunzi saba kati ya 10 bora kwenye mtihani huo walichagua kusomea kozi ya udaktari katika vyuo mbalimbali nchini.
Kijumla, wanafunzi 155 kati ya 314 ambao walipata alama ya ‘A’ katika mtihani huo walichagua kusomea kozi ya udaktari.
Mwanafunzi Otieno Teddy Odhiambo ambaye aliibuka bora katika mtihani huo atasomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Wengine watakaosomea kozi hiyo katika chuo hicho ni Edwin Otieno Ouko, Ian Kiplagat, Matsotso Madlean Auma na Mathenge Stephanie Kirigo. Whitney Nicanor Mabwi, aliyekuwa wa nane bora atasomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Moi.
Kozi zingine zilizoibuka kuwa maarufu miongoni mwa wanafunzi ni somo la uchumi, uhandisi wa barabara, sayansi ya kompyuta, uhandisi wa ndege, upasuaji wa meno, sheria, sayansi ya bima na somo la utaalamu wa dawa.
Msisitizo wa serikali kwa wanafunzi kuegemea masomo ya sayansi na teknolojia pia ulionekana kukumbatiwa na wengi, kwani kati ya wanafunzi 89,486 waliohitimu kujiunga na vyuo vikuu, 57,687 walichagua kozi zinazohusiana na hayo. Idadi hiyo inawakilisha asilimia 64 ya wanafunzi wote.
Kati ya hao, 36,189 ni wavulana huku 21, 498 wakiwa wasichana.
Akitoa ripoti hiyo, Prof Magoha alisema kuwa lazima wanafunzi watilie maanani umuhimu wa kozi wanayochagua kusomea.
“Wanafunzi lazima wafanye utafiti wa kina ili kubaini umuhimu wa kile wanachoenda kusomea katika vyuo vikuu, hasa kutokana na ushindani mkubwa uliopo,” akasema.
Chuo Kikuu cha Nairobi pia kiliibukia kupendelewa na wanafunzi wengi zaidi, kwani kati ya wanafunzi 314 waliopata alama ya ‘A’ 191 watajiunga na chuo hicho.
Chuo hicho kimekuwa kikiorodheshwa kuwa bora nchini na ukanda wa Afrika Mashariki na mashirika mbalimbali ya utafiti. Chuo pia kimesifiwa kwa ubora wa kozi zake.
Prof Magoha aliitaka Tume ya Elimu ya Juu (CUE) kufanya utathmini wa kina kuhusu ubora wa kozi ambazo zinatolewa katika vyuo vikuu nchini kwani kozi tisa hazikuchaguliwa na mwanafunzi yeyote katika vyuo vikuu.
Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa kozi 98 hazitapata mwanafunzi yeyote, kwani wengi waliotuma maombi kuzisomea hawakufikisha viwango vinavyohitajika.
Baadhi ya kozi hizo ni sayansi ya mazingira, usimamizi wa hoteli, sayansi ya mawasiliano, ualimu wa chekechea, sayansi ya mchanga, utaalamu wa chakula, usimamizi wa misitu kati ya zingine
Kulingana na Prof Magoha, baadhi ya matatizo yanayoandama mfumo wa utoaji kozi ni ukosefu wa utafiti wa kutosha kuhusu manufaa yake na ushindani usiofaa miongoni mwa vyuo vikuu.
Kando na hayo, vyuo mbalimbali vinatoa kozi zinazofanana, bila kuzingatia viwango vinayolingana na mahitaji ya kisasa.
Vile vile, baadhi ya kozi ambazo hazikupokea ombi la mwanafunzi yeyote ni zile kuhusu somo la dini, ustawishaji wa jamii, utatuzi wa mizozo, usimamizi wa biashara, sayansi ya mazingira kati ya zingine.