Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mazingatio makuu katika ufunzaji wa ufupisho

April 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

UFUPISHO ni mojawapo ya mihimili muhimu katika ufundishaji wa uandishi wa muhtasari.

Kimsingi, kipengele hiki muhimu huwa kinatahiniwa katika Karatasi ya Pili ya Kiswahili (102/2) katika Mtihani wa Kitaifa wa Kuhitimu Elimu ya Sekondari nchini Kenya (KCSE).

Baadhi ya madhumuni muhimu ya kufundisha muhtasari ni: kuwawezesha wanafunzi kuelewa makala au taarifa iliyotolewa, kisha kuteua kilicho muhimu ili kuwasilisha ujumbe wa makala au taarifa hiyo kwa ufupi na kwa njia inayoeleweka.

Lengo kuu hasa ni kuwapa wanafunzi ustadi utakaowawezesha kukabiliana na majukumu yatakayohitaji ufupishaji katika maisha yao, kwa mfano: ufupishaji wa makala, barua za ofisini na uandishi wa matangazo.

Ili kufanikiwa, ufupisho unahitaji kunga zifaazo: (i) Ufahamu wa sentensi, aya na makala/taarifa (ii) Kuainisha/ kuteua kilicho muhimu katika makala, taarifa fulani, aya au hata sentensi (iii) Kuelewa msamiati uliotumiwa katika makala na maana kama inavyojitokeza katika muktadha (iv) Kuelewa jinsi matukio fulani yanavyosababisha matukio mengine au jinsi hali moja inavyosababisha hali nyingine (v) Kuelewa jinsi matukio au hoja zinavyofuatana (vi) Kuelewa uhusiano uliopo wa mambo mbalimbali katika makala.

Vigezo hivyo huwa mhimili muhimu katika ujenzi wa hatua nne zifuatazo kwenye uandishi wa ufupisho:

Uuunganishi wa hoja katika mtungo wa ufupisho

(i) Mambo muhimu katika kipengele hiki ni kwamba utungo wa ufupisho humhitaji mwanafunzi kueleza habari fulani kwa ufupi kadri iwezekanavyo, hasa kwa kuzingatia idadi ya maneno yanayohitajika

(ii) Mwanafunzi anahitajika kujieleza waziwazi kwa njia ambayo inaweza kueleweka vizuri na msomaji

(iii) Hoja zinatakiwa kupangwa kwa mtiririko na kwa njia ambayo itazifanya zionekane, zieleweke kwa urahisi na zikumbukwe pia.

Uteuzi wa makala za kufanyia ufupisho

Katika kipengele hiki, mwalimu anapaswa kufahamu namna anavyoweza kuchagua makala za kufanyia ufupisho. Baadhi ya hoja zitakazomsaidia ni kama:

(i) Makala zilizochaguliwa ziwe zafaa kwa ufupisho. Makala yaweza kuwa na hoja mbalimbali, matukio mbalimbali, maagizo au maoni. Si vizuri kutegemea makala zinazohusu hadithi, ngano au visa, mashairi na maelezo ya kubuni.

(ii) Makala inayoeleweka kwa urahisi bila matatizo mengi na inayopendeza itafaa zaidi kwa ufupisho kuliko makala ngumu.

(iii) Mazoezi ya ufupisho yanaweza kufanywa kutokana na vitabu, hotuba, majadiliano na hata kumbukumbu za mikutano

Namna mwalimu anavyoweza kuwasaidia wanafunzi wake kujifunza ufupisho

(i) Mwalimu anaweza kuwataka wanafunzi kuisoma makala au taarifa fulani kimya kimya

(ii) Mwalimu na wanafunzi wake waipitie makala na kujadili maana yake kwa jumla.

(iii) Baada ya majadiliano mwalimu anaweza kuwataka wanafunzi kuonyesha ubaoni au katika karatasi maneno au hoja muhimu.

(iv) Makala itakayounganisha hoja zilizo muhimu inaweza kuandikwa ubaoni au katika madaftari ya wanafunzi. Ikiandikwa ubaoni, itabidi mwalimu kuwaita wanafunzi wake tofauti tofauti mbele ili wajaribu kuirekebisha mpaka pale mwalimu atakaporidhikakuwa makala yote yameandikwa vizuri.

Mazoezi ya ufupisho

Njia zifuatazo zinaweza kutumiwa ili kukuza ustadi wanafunzi wa kufanya muhtasari:

(i) Wanafunzi wanaweza kupewa aya kisha wakapewa sentesi kadhaa ambazo miongoni mwazo watatambua ni zipi zinazowakilisha aya au makala iliyotolewa.

(ii) Wanafunzi wanaweza kupewa aya au makala iliyo na mapengo yaliyoachwa kisha watakakiwe kuzikamilisha kwa kutumia maneno mwafaka.

(iii) Wanafunzi wapewe taarifa fupi fupi au aya kisha watakiwe kuiandikia muhtasari wa sentensi moja au mbili.

(iv) Wanafunzi watakiwe kusoma taarifa kisha wajibu maswali kadhaa wakitumia idadi ya maneno inayohitajika.

(v) Wanafunzi watakiwe kusoma makala au taarifa kisha watoe kichwa kinachofaa habari hiyo.

(vi) Wanafunzi waombwe kufupisha matangazo ya vifo, biashara au mikutano ya yatakayotokea katika magazeti.

Kimsingi, ufupisho ni nyenzo kuu ambayo huhakikisha kuwa mwanafunzi anafanikiwa katika nyanja muhimu za uandishi kama uanahabari.

Katika uandishi wa habari, mwanafunzi hutumia ujuzi wa ufupisho, kwani huwa haandiki matini zote, bali hunakili hoja zilizo muhimu ambazo baadaye huzitumia katika uandishi wa nakala yake ya mwisho.

Kijumla, kipengele hiki ni muhimu sana, si kwa wasomi wa Kiswahili pekee, bali kwa kila mmoja kwani huwa tunakumbana na uandishi wa matini katika kila nyanja ya maisha.

 

[email protected]