• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
Shujaa yaomba kukwepa shoka Raga ya Dunia

Shujaa yaomba kukwepa shoka Raga ya Dunia

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya almaarufu Shujaa imerejea nyumbani salama salmini kutoka Singapore ikiwa na matumaini makubwa itakwepa kuangukiwa na shoka kwenye Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019.

Katika mahojiano Jumanne, nahodha Jeffrey Oluoch amesema mwezi mmoja wa maandalizi walionao kabla ya duru mbili za mwisho utawapa nguvu zaidi kupambana na miamba Fiji na Samoa pamoja na Ufaransa katika mechi za Kundi B wakilenga kufika robo-fainali yao ya kwanza kuu msimu huu jijini London mnamo Mei 25-26 nchini Uingereza.

“Tuko katika kundi la kusisimua, lakini kali, ingawa naamini mwezi mmoja wa maandalizi kabla ya kuelekea jijini London utatutosha kuimarisha sehemu tuna nguvu na kurekebisha zile ambazo tulikuwa na ulegevu. Lengo letu bado linasia kufika robo-fainali kuu.

“Ni kweli tunakabiliwa na presha. Ili kupunguza presha hii, tunahitaji kufungua mwanya mzuri kati yetu na timu mbili za mwisho kwa kufika robo-fainali. Kwa sasa, tuko alama moja mbele ya Wales na nne pekee juu ya Japan,” alisema.

Kenya imekuwa timu inayoshiriki duru zote za Raga ya Dunia tangu msimu 2002-2003. Hata hivyo, msimu huu wote imekuwa ikining’inia pabaya tangu imalize duru ya ufunguzi katika nafasi ya mwisho mjini Dubai mnamo Desemba 1, 2018.

Ni mara ya pili katika misimu minane Kenya inakabiliwa na hatari ya kutemwa baada ya kuponea tundu la sindano msimu 2011-2012 ilipomaliza mkiani katika nafasi ya 12, lakini kwa bahati nzuri idadi ya washiriki wa msimu 2012-2013 ikaongezwa na Shirikisho la Raga Duniani hadi 15.

Katika msimu huu, vijana wa Paul Murunga walirejea kutoka ziara ya Bara Asia na alama nane baada ya kuzoa tano mjini Hong Kong na tatu nchini Singapore.

Wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 26 baada ya duru nane za kwanza, alama moja mbele ya nambari 14 Wales na pointi nne juu ya Japan inayoshikilia nafasi ya 15, ile ya kutemwa.

Timu itakayovuta mkia baada ya duru mbili za mwisho kusakatwa mijini London (Mei 25-26) na Paris, Ufaransa (Juni 1-2) itapoteza nafasi yake kwenye raga hii ya kifahari.

Katika tathmini yake ya duru ya Hong Kong Sevens, Oluoch alisema kwamba hakukuwa na mshikamano mzuri kati ya wachezaji wazoefu waliokuwa wanarejea kikosini (Andrew Amonde, Augustine Lugonzo, Nelson Oyoo, Eden Agero na Daniel Sikuta), na chipukizi ambao wamekuwepo tangu duru ya Dubai.

Wachezaji wazoefu walisusia duru sita za kwanza wakilalamikia kupunguzwa mishahara. “Mshikamano huu uliimarika kidogo nchini Singapore, ingawa matokeo hayakudhihirisha hivyo,” aliongeza Oluoch.

Kuhusu hofu ya uwezekano wa Kenya kuangukiwa shoka, Oluoch alisema, “Kenya haitatemwa. Hata hivyo, kuepuka masaibu hayo, lazima tuimarishe ulinzi wetu, unyakaji wa mipira inapoanzishwa na umiliki wa mpira na pia kuimarisha jinsi timu inacheza kwa jumla.

Hii itatuwezesha kupata alama zitakazotuondolea presha inayokuja kutoka kwa Wales na Japan. Mabingwa hawa mara nne wa Afrika wameratibiwa kurejelea mazoezi mapema juma lijalo, lakini bila wachezaji Lugonzo, Oyoo na Oscar Dennis ambao waliumia kumbo, kifundo na goti nchini Singapore mtawalia.

Msimamo wa Raga ya Dunia ya 2018-2019 baada ya duru nane za kwanza:

Nchi Pointi

Marekani 145

Fiji 142

New Zealand 130

Afrika Kusini 121

Uingereza 107

Samoa 87

Australia 80

Argentina 79

Ufaransa 71

Scotland 62

Uhispania 47

Canada 41

Kenya 26

Wales 25

Japan 22

You can share this post!

Thika Queens na Vihiga Queens wamumunya wapinzani

IEBC yatuma wawakilishi katika uchaguzi wa wanachuo wa...

adminleo