• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Ndani kwa mashtaka ya kubambwa wakiwa na ‘dhahabu’

Ndani kwa mashtaka ya kubambwa wakiwa na ‘dhahabu’

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wanne wa Rwanda na Wakenya wawili walikifishwa kortini Jumanne kwa tuhuma walipatikana na dhahabu feki.

Washukiwa hao waliotiwa nguvuni Jumanne asubuhi katika eneo la Yaya Centre, Nairobi waliamriwa na Hakimu mwandamizi Bi Muthoni Nzibe wazuiliwe kwa siku tatu kuwasaidia polisi kukamilisha uchunguzi.

Afisa anayechunguza kesi dhidi ya Niyitegeka Sevelin, Dushimiriamana Egide, Zilimwabagabu Jacrues , Ngaragura Emmanuel na Wakenya Grace Wairimu Machatha na Erascos Katiku Josiah alisema washukiwa hao walipatikana wakiwa na sanduku ya madini yanayodhaniwa kuwa dhahabu.

“Naomba washukiwa wazuiliwe kwa siku 10 kwa vile madini haya yanatakiwa kupelekwa kwa maabara ya idara ya madini kuchunguzwa ikiwa ni dhahabu au la,” alisema Bw Alfa Ochieng.

Mahakama ilifahamishwa kuwa raia hao wa Rwanda hawakuwa na vitambulisho na watapelekwa idara ya Uhajiami ibainike ikiwa wamo nchini Kenya kihalali.

Wakili Stanley Kang’ahi anayewatetea washukiwa hao alisema hakuna ushahidi wowote ambao polisi wamewasilisha kuonyesha washukiwa wakiachiliwa watatoroka.

“Kuwazuia kwa siku 10 ni kukandamiza haki zao,” Bw Kang’ahi alimweleza hakimu.

Aliomba siku hizo zipunguzwe hadi siku mbili au tatu kuwezesha polisi kuwasiliana na idara ya uhamiaji kuhoji ikiwa raia hao wa Rwanda wako na hati za kuwawezesha kuishi nchini.

Washtakiwa warudishwa kortini Ijumaa.

You can share this post!

Meneja wa Kenya Power asukumwa kwa kona

Polisi watatu kizimbani kwa kumtisha mfanyabiashara

adminleo