• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Uhuru na Raila wasusia kongamano la madiwani Kisumu

Uhuru na Raila wasusia kongamano la madiwani Kisumu

Na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wamesusia kongamano la madiwani linalokamilika Jumatano jijini Kisumu, wakiwaacha washiriki bila kuelewa sababu ya hatua yao.

Rais Kenyatta alitarajiwa kufungua rasmi kongamano hilo linalofanyika katika hoteli ya Grand Royal Swiss Jumatatu, lakini alimtuma waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa.

Bw Wamalwa, hata hivyo, hakuwa na hotuba ya Rais, ila alisoma hotuba yake, ambayo alikuwa ameandaa.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga naye alitarajiwa kuhudhuria na kuhutubia kongamano hilo jana alasiri, japo hakuonekana.

Bw Odinga aidha hakumtuma kiongozi yeyote kumwakilisha, ila badala yake jana alikuwa akiendesha kongamano jingine Jijini Nairobi kuhusu masuala ya miundomsingi barani Afrika.

Bw Odinga, hata hivyo, amekuwa akiwashutumu Wawakilishi wa Wadi kuwa wanalemaza ugatuzi, huku Desemba mwaka jana akisema idadi yao inafaa kupunguzwa kwani hawawakilishi wananchi ipasavyo.

Kongamano hilo limewaleta pamoja madiwani, maspika na viongozi wengine wa kaunti, viongozi wa bunge la seneti wakihusisha spika Kenneth Lusaka, Kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen na wa wachache James Orengo.

Kutojitokeza kwa viongozi hao wawili, ambao walitarajiwa kwa hamu kabla ya kuanza kwa kongamano hilo kuliwaacha wengi bila kujua sababu yao kuamua kulisusia, wakati wito ulitolewa kuwa kamati iundwe ya kuhakikisha kuwa yanayojadiliwa yanatekelezwa.

Maseneta wakiongozwa na Spika Lusaka, Bw Murkomen na Bw Orengo ndio waliongoza wito huo. “Kuna haja ya kuwa na kamati maalumu itakayofuatilia utekelezwaji wa mambo yanayojadiliwa la sivyo huu utakuwa mkutano wa kujifurahisha tu,” akasema Bw Lusaka.

Naibu Rais William Ruto naye anatarajiwa kulifunga kongamano hilo, japo haijulikani ikiwa atafika.

You can share this post!

Afisi ya DCI ina mamlaka ya kuchunguza kesi za ufisadi...

Wabunge wadai muungano mpya wa kisiasa watokota 2022

adminleo