Maelfu hatarini kupigwa kalamu vyuoni
Na OUMA WANZALA
MAELFU ya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu wako katika hatari ya kufutwa kazi baada ya wanafunzi waliohitimu mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) kukataa jumla ya kozi 107.
Kulingana na Bodi ya Kugawa Wanafunzi Vyuoni (KUCCPS), kozi 107 zinazohusiana na mazingira, theolojia, kilimo na uvuvi zilikosa wanafunzi.
Jumanne, Tume ya Elimu ya Chuo Kikuu (CUE) na manaibu chansela wa vyuo vikuu walisema watawatimua wafanyakazi na wahadhiri waliokuwa wakifunza kozi zilizokataliwa na wanafunzi.
Katika Chuo KIkuu cha Kisii, kozi nne hazitakuwa na wanafunzi mwaka huu.
Kozi zilizokataliwa ni Digrii ya Masomo ya Amani na Mizozo, Digrii ya Usimamizi wa Biashara, Digrii ya Rasilimali za Majini na Digrii ya Maliasili.
Vyuo vikuu vya Presbyterian na Nazarene havitakuwa na wanafunzi wanaosomea kozi ya dini au theolojia.
Chuo Kikuu cha Cooperative University of Kenya (KCA) hakitakuwa na wanafunzi wanaosomea kozi ya Elimu ya Huduma kwa Jamii.
Kozi ya Hewa Safi haitafunzwa katika Chuo Kikuu cha Kirinyaga kutokana na ukosefu wa wanafunzi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Manaibu Chansela wa Vyuo Vikuu vya Umma Francis Aduol jana alisema kuwa wafanyakazi kutoka idara zisizo na wanafunzi watafukuzwa.
“Wahadhiri waliokuwa wakifundisha kozi zilizokataliwa watalazimika kwenda. Chuo husika kitaamua hatima ya wafanyakazi wengine waliokuwa wakihudumu katika idara zilizoathiriwa,” akasema Profesa Aduol.
Alisema hatua ya wanafunzi kukataa kozi hiyo ni ishara kwamba, hazina manufaa na zinafaa kufutiliwa mbali.
Prof Aduol alisema vyuo vikuu vinafaa kulaumiwa kwa kubuni kiholela kozi zisizokuwa na manufaa.
Mwenyekiti wa CUE Chacha Nyaigoti Chacha (pichani juu) alivitaka vyuo vikuu kufutilia mbali kozi ambazo hazijakuwa zikipendelewa na wanafunzi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
“Itakuwa vigumu kwa vyuo vikuu kuendelea kulipa mishahara wahadhiri wa kozi zisokuwa na wanafunzi,” akasema Prof Nyaigoti.
Lakini, Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Scott Christian, Mumo Kisau ambaye pia ni mwenyekiti wa muungano wa Vyuo Vikuu vya Kibinafsi, alisema hakuna haja ya kuwa na wasiwasi.
Chuo Kikuu cha Scott Christian ni miongoni mwa vyuo vikuu ambavyo vitakosa wanafunzi wa somo la theolojia mwaka huu.
“Kozi ya theolojia zinalenga watu wazima waliokomaa na wala si vijana wadogo waliokamilisha elimu ya Kidato cha Nne,” akasema Prof Kisau.
Vyuo vikuu tayari vimependekeza kupandisha ada inayotozwa wanafunzi, hatua ambayo imepingwa vikali na wazazi kwamba inalenga kufungia nje wanafunzi kutoka familia maskini.
Wizara ya Elimu imekuwa ikivitaka vyuo vikuu kufunza kozi zinazowawezesha kupata ajira baada ya kuhitimu masomo yao.
Mnamo Jumatatu, Waziri wa Elimu George Magoha aliagiza tume ya CUE kuanzisha uchunguzi kuhusu ufaafu wa kozi zilizokosa wanafunzi.
“Jambo la kushangaza ni kwamba, baadhi ya vyuo vikuu vinafunza kozi tofauti zinazokaribiana,” akasema Prof Magoha.