• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
GWIJI WA WIKI: Winnie Anne Otieno

GWIJI WA WIKI: Winnie Anne Otieno

Na CHRIS ADUNGO

SUBIRA ni miongoni mwa siri kubwa za kufanikiwa kwa mtu maishani na kitaaluma. Haiwezekani kabisa kwa mambo yote kuja kwa wakati mmoja.

Ufanisi ni zao la bidii, nidhamu, imani na stahamala.

Milango ya heri hujifungua yenyewe kwa watu wenye sifa hizi. Chagua maono yenye matarajio na uanze kuota ndoto zenye thamani ili maazimio yako yatimie. Jifunze kutokata tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo kisha teua kushindana na wakati.
Thamini hicho unakichokifanya, jitahidi kuwa mbunifu na waulize wajuao zaidi yako. Pania sana kujiboresha katika chochote unachokitenda huku ukijiwekea malengo mapya ya mara kwa mara.
Huu ndio ushauri wa Bi Winnie Anne Otieno – Afisa Mkuu Msaidizi na mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Starehe Boys Centre, Nairobi.

Maisha ya awali

Bi Winnie alizaliwa mnamo 1990 katika mtaa wa Chaani, eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa. Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto wawili wa marehemu Bi Josephine Awiti ambaye hadi kufariki kwake mnamo 1998, alikuwa mfanyakazi katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Moi, Mombasa.

Alianza safari yake ya elimu katika Chekechea ya Holy Ghost Catholic Chaani kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Umoja, Mikindani alikosomea kati ya 1997 na 1998.

Kufa kwa wazazi wa Winnie kulitikisa ulimwengu wake pakubwa na kuzamisha nyingi za ndoto alizokuwa nazo utotoni.

Kwa imani kwamba penye mawimbi na milango i papo hapo, alianza kuishi na mjomba wake Charles Otieno jijini Mombasa.

Hata hivyo, mshumaa wa matumaini yaliyoning’inizwa kwenye uzi mwembamba wa imani ulionekana kuzimika tena pindi Bw Otieno alipoaga dunia mwezi mmoja baadaye.

Mnamo 1999, Winnie alitwaliwa na halati yake Bi Agnes na akajiunga na Shule ya Msingi ya Assar Johansson, Migori akiwa mwanafunzi wa Darasa la Nne.

Alama nzuri alizozipata katika mtihani wa KCPE mnamo 2003 zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya St Mary’s Gorretti Dede Girls katika eneo la Rongo, Migori.

Ukakamavu, bidii masomoni na nidhamu ya hali ya juu ni miongoni mwa sifa zilizomfanya ateuliwe kuwa Naibu Kiranja Mkuu akiwa mwanafunzi wa Kidato cha Tatu.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2007 na akawa miongoni mwa wanafunzi waliotia fora zaidi katika masomo ya Dini, Kiswahili, Kiingereza, Jiografia na Bayolojia.

Aliibuka mwanafunzi wa tatu bora katika shuleni St Marys.

Winnie anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa walezi wake ambao walimhangaikia katika kila hali, kumwelekeza ipasavyo na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Wengine waliomshajiisha zaidi kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hiyo ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi; ni Bw Ngei, Bw Midam na Bi Kaunda waliompokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya upili.

Mtihani mgumu zaidi aliokabiliana nao baada ya kukamilisha mtihani wa KCSE ni vita vya ndani ya nafsi vilivyompa msukumo wa kutaka kuwa ama rubani au mwanahabari licha ya wengi wa marafiki zake kumshauri ajitose kikamilifu katika ulingo wa sanaa ya uigizaji.

Mengi ya maigizo aliyoyashiriki shuleni yalimzolea sifa na kumvunia umaarufu miongoni mwa mwenzake.

Isitoshe, ufundi mkubwa katika tungo alilzozisuka ni upekee uliompandisha kwenye majukwaa ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa na za kutamanika mno katika ulingo wa Kiswahili.

Akiwa na umri wa miaka 17 pekee, alipata kibarua cha kuuza nguo katika mojawapo ya maduka mjini Migori. Alianza baadaye kuuza vitabu kabla ya kuwa mhudumu wa duka la M-Pesa.

Usomi na kazi

Ilikuwa hadi Oktoba 2009 alipojiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta jijini Nairobi kusomea Shahada ya Ualimu katika Kiswahili na Jiografia. Anawastahi sana wahadhiri waliofanikisha safari yake ya elimu chuoni, hasa Dkt Miriam Osore na Dkt Hamisi Babusa ambao walimrithisha ilhamu na kariha ya kukichapukia Kiswahili alaa kulihali.

Wawili hawa walimchochea Winnie na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha mapenzi ya dhati kwa masomo ya lugha.

Utashi na motisha zaidi ilitoka kwa wanafunzi wenzake waliokuwa wakimpongeza kwa umilisi wake wa Kiswahili na upekee wa kiwango chake cha ubunifu katika utunzi wa mashairi ya Kiswahili na Kiingereza.

Akiwa chuoni, Winnie alitambua pia utajiri wa kipaji chake katika sanaa ya ulumbi.

Aliwahimiza wanafunzi wengi kushiriki mashindano ya uigizaji na kughani mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa na Winnie kwa sasa katika ulingo wa Kiswahili ni zao la yeye kufundishwa na wasomi ambao mbali na kubobea ajabu kitaaluma, pia waliipenda na kutawaliwa na ghera ya kuipigia chapuo lugha hiyo.

Hadi alipofuzu kuwa mwalimu mnamo Julai 2013 Winnie alikuwa amesomea pia Diploma katika masuala ya uajiri na usimamizi wa maslahi ya wafanyakazi kutoka Kenya Institute of Management (KIM).

Baada ya kufanya kazi ya kujitolea kwa miezi sita shuleni Starehe Boys Centre, Winnie alipata ajira ya kufundisha Kiswahili katika Kambi ya Wakimbizi ya Dadaab, Garissa chini ya udhamini wa Shirika la Windle Trust International (WTI).

Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitatu kati ya 2013 na 2015.

Mbali na kuwapenda na kuwathamini wanafunzi wake wote, Winnie aliwaamshia ari ya kuthamini na kulichapukia somo la Kiswahili licha ya kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi hao walikuwa wazawa wa Sudan na Somalia.

Anakiri kwamba kuhudumu kwake Dadaab kulimwekea msingi imara wa ualimu licha ya changamoto za kila sampuli.

Mnamo 2015 Winnie aliajiriwa kuwa Afisa Mkuu Msaidizi wa Mkurugenzi wa Shule ya Upili ya Starehe Boys Centre.

Katika wadhifa wake, anashughulikia masuala ya mawasiliano na uteuzi wa wanafunzi wanaotokea katika familia zisizojiweza kwa minajili ya kudhaminiwa shuleni humo na katika vyuo vikuu vya kigeni.

Ilikuwa hadi Mei 2015, ambapo alianza kufundisha Kiswahili shuleni Starehe Boys Centre na kuwashirikisha wanafunzi wake kwa Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti la Taifa Leo.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaojivunia kila mara matokeo ya mitihani ya kitaifa ya KCSE yanapotolewa.

Msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ulimchochea kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 2017 kusomea shahada ya Uzamili katika masuala ya elimu na usimamizi.

Anatarajia kufuzu mwishoni mwa mwaka 2019.

Kipi amajivunia?

Winnie anajivunia kuhudhuria makongamano mbalimbali katika maeneo ya Kaskazini Mashariki ya Kenya kwa nia ya kuchangia makuzi ya Kiswahili na kuwatia hamasa watoto wa kike.

Hili ni jambo ambalo amekuwa akilifanya kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Aidha, anajivunia kuchangia kishujaa uendeshaji wa kipindi ‘Mawimbi ya Lugha’ katika runinga ya KU-TV.

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kudumisha uhai wa ndoto za kuwa mhadhiri wa chuo kikuu, anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wanafunzi ambao kwa sasa ni wataalamu wanaoshikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

You can share this post!

MAPISHI: Pancakes

KAULI YA MATUNDURA: Yasikitisha wanafunzi wa kisasa vyuoni...

adminleo