Bravin Kipkosgei na Vincent Kibet washindia Kenya dhahabu Riadha za U-18 na U-20
Na GEOFFREY ANENE
Kenya ilianza mashindano ya Riadha za Afrika za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 na 20 kwa kishindo baada ya Bravin Kipkosgei na Vincent Kibet kutwaa mataji ya mita 10,000 na mita 1,500 mjini Abidjan, Ivory Coast mnamo Jumanne.
Kipkosgei aliongoza Mkenya mwenzake Emmanuel Korir kunyakua medali ya dhahabu na shaba katika kitengo hicho cha mizunguko 25.
Kenya sasa ina jumla ya medali sita baada ya Kibet kuongoza Peter Kibui kuvuna dhahabu na shaba mtawalia katika mbio za mita 1,500 za wakimbiaji wasiozidi umri wa miaka 18.
Janet Nyiva na Emmaculate Akinyi walishindia Kenya nishani za fedha katika mbio za mita 1,500 na mita 3,000 katika mashindano ya Under-18 na Under-20 mtawalia.
Keter alikamilisha mbio za mita 1,500 kwa dakika 3:40.28 akifuatwa na Muethiopia Fentahun Gezahignyihun (3:43.64) naye Kibui akafunga tatu-bora kwa 3:45.50.
Nyiva alimaliza mita 1,500 za Under-18 kwa dakika 4:20.43. Mmoroko Meryem Azrour alinyakua dhahabu kwa dakika 4:20.14 naye Muethiopia Girma Tilahunalmaz akaridhika na shaba (4:21.97).
Mkenya Maureen Cherotich alikamilisha katika nafasi ya nne (4:24.09).