Kalonzo awataka wabunge wa chama chake kuhepa Sifuna
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amewataka viongozi wa chama hicho waliokuwa wakizunguka na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuvumisha vuguvugu la Linda Mwananchi kurejea katika shughuli za Wiper, huku mvutano ndani ya upinzani ukizidi kushika kasi kuelekea uchaguzi wa 2027.
Akizungumza Mombasa wakati wa ziara yake ya siku mbili, Bw Musyoka alisema ushirikiano kati ya Wiper na chama ambacho Bw Sifuna atakuwa nacho utakuwa katika kiwango cha muungano, akisisitiza kuwa wanachama wa Wiper wanapaswa kuimarisha chama chao.
“Leo tuko Mombasa na mnaweza kuona Joshua Kimilu wa Kaiti na Mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako, ambao wamekuwa wakizunguka na Bw Sifuna, wameitwa kurejea. Tunatarajia sasa wajikite katika shughuli za Wiper na kuacha Bw Sifuna kuvumisha chama chake tukutane katika kiwango cha muungano,” alisema.
Kauli hiyo inajiri huku Bw Sifuna na wafuasi wake wakipanga kubadilisha jina la chama cha Equitable Party ndani ya wiki tatu, baada ya kukosa fursa ya kutumia jina la Ukombozi. Washirika wa Bw Musyoka walihifadhi jina hilo na kulitumia kuunda muungano wa The Ukombozi Alliance.
Mzozo huo unaonyesha changamoto inayokabili viongozi wa upinzani wanaotaka kuunganisha nguvu dhidi ya Rais William Ruto, huku kila upande ukijenga chama chake na kutafuta ushawishi katika mazungumzo ya kuunda muungano kuelekea uchaguzi.
Bw Musyoka pia anapanua kampeni zake Pwani, eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa ngome ya ODM. Alidai kuwa chama hicho hakijawatendea haki wakazi wa eneo hilo na akawahimiza kuunga mkono Wiper katika uchaguzi mkuu ujao.
“ODM imekuwa ikiwachezea watu wa Pwani. Wiper imekuja kuwaokoa wakazi. Tutaingia na kushinda kura nyingi zaidi tunapoelekea uchaguzi wa urais,” alisema.
Ziara yake inafuatia ile ya Rais Ruto ya siku nane Pwani, ambako alitangaza miradi ya maendeleo na kugawa hati za umiliki wa ardhi.
Kiongozi huyo wa Wiper pia alitaja kuondoka kwa Seneta wa Nakuru Tabitha Karanja kutoka chama cha UDA na kujiunga na DCP kama ishara ya kutoridhika ndani ya chama tawala.
Alitabiri kuwa viongozi wengine wataondoka UDA kabla ya uchaguzi wa 2027, ingawa bado haijabainika ikiwa hatua hizo zitasababisha wimbi kubwa la mabadiliko ya kisiasa.
Wakati huo huo, viongozi wa upinzani wamepinga mageuzi yanayopendekezwa katika mashirika ya umma, hasa Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) na Kampuni ya Bomba la Mafuta Kenya (KPC), wakidai kuwa yanaweza kuhatarisha ajira na mali ya umma.
Bw Musyoka ameandamana na viongozi wa upinzani akiwemo Justin Muturi, Eugene Wamalwa na Mbunge wa Nyali Mohamed Ali, ambaye anawania ugavana Mombasa.