• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Njia faafu ya kulitanguliza somo la Fasihi Andishi kwa wanafunzi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Njia faafu ya kulitanguliza somo la Fasihi Andishi kwa wanafunzi

Na CHRIS ADUNGO

KABLA ya kuwatanguliza wanafunzi katika somo la Fasihi Andishi na kuanza kusoma kitabu chochote kile, ni vyema kwa mwalimu kuwaandaa wanafunzi wake vilivyo ili wajue kwa kina istilahi zote za kifasihi.

Baadhi ya istilahi hizi muhimu na za msingi ni Riwaya, Tamthilia na Hadithi Fupi.

Ni vyema pia kwa mwalimu kuwafafanulia wanafunzi wake sifa za kila mojawapo ya tanzu za hapo juu.

Katika sehemu zitakazofuata, mwalimu atalazimika kuwaelezea wanafunzi dhana na maana ya Dhamira na Maudhui na jinsi ya kutambua na kung’amua vipengele hivyo katika kazi mbalimbali watakazozizamia.

Baada ya kutambua wahusika ni nani katika kazi husika ya Fasihi Andishi, hatua muhimu inayostahili kuzingatiwa na wanafunzi kwa ushirikiano na mwalimu ni kuwaainisha wahusika wenyewe.

Mwalimu awaelekeze wanafunzi kuhusu jinsi ya kuzitambua sifa tofauti za wahusika na kufafanua umuhimu wa kila mmoja wao katika kujenga ploti, kukuza maudhui, kuendeleza dhamira na kudhihirisha sifa za wenzao.

Itakuwa vyema pia kwa mwalimu kushirikiana na wanafunzi kubainisha mbinu mbalimbali za uandishi na za lugha ambazo zimetumiwa na waandishi wa kazi wanazozishughulikia.

Anapotoa maelezo ya kila mojawapo ya mbinu hizo, mwalimu anastahili kutumia mifano mbalimbali hata kutoka katika vitabu vingine tofauti na vile teule ambavyo wanafunzi wake wanavisoma kwa wakati huo.

Baada ya hayo yote, wanafunzi watakuwa na hamu hata zaidi ya kujisomea kazi za kila sampuli.

Kabla mwalimu kuanza usomaji wa vitabu teule vya Fasihi Andishi, anapaswa kuhakikisha kuwa asilimia 75 hadi 100 ya wanafunzi wake wana vitabu vyao binafsi.

Kuna njia mbili za usomaji: Mwalimu kuwasomea wanafunzi wake kitabu husika kwa sauti ya juu huku akitua mara kadhaa na kufafanua sehemu tata.

Pili, wanafunzi wasome kwa zamu au kwa kupokezana huku mwalimu akichukua nafasi ya unahodha kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anashiriki usomaji wa kiasi fulani cha kurasa.

Mbinu zote mbili zina umuhimu na taksiri zake. Katika ile ya kwanza, mwalimu anaweza kumaliza usomaji haraka lakini baadhi ya wanafunzi wasielewe chochote kabisa mwishoni mwa usomaji huo.

Ya pili ingekuwa njia bora ambayo ingempa kila mwanafunzi jukwaa la kushiriki kikamilifu, lakini baadhi ya wanafunzi hawajakirimiwa uwezo wa kusoma kwa kasi.

Hivyo, usomaji huenda ukachukua muda mrefu zaidi kuhitimisha. Ingawa hivyo, itakuwa vyema zaidi kwa mwalimu kutumia mbinu zote mbili kwa pamoja.

Wakati wa kusoma, mwalimu anatakiwa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi ana kalamu ya risasi au penseli ili apigie vistari mbinu za lugha na sanaa na kuandika kwa maelezo mafupi muhimu kando ya kurasa za kitabu chake.

Baada ya kila sura, tendo au onyesho, mwalimu ahakikishe kwamba amewatungia wanafunzi wake maswali rahisi ili wakumbuke kabisa mtiririko wa visa katika sehemu hizo walizozipitia pamoja.

Maswali yotolewe kutoka sehemu zenye migogoro kati ya wahusika kitabuni au zile zilizo na mbinu mbalimbali za uandishi. Mfano wa maswali ya kutunga ni: Weka dondoo hili katika muktadha. Fafanua ukweli wa kauli hii ukirejelea riwaya, hadithi fupi au tamthilia.

Ni mbinu gani iliyotumika katika dondoo hili? Eleza sifa za mnenaji, mnenewa au mrejelewa. Mwalimu anapaswa kuwaachia wanafunzi wake maswali haya ili wayachambue wenyewe kisha katika kipindi kinachofuata, awaletee majibu au awaongoze kuyajadili majibu yao.

Akitumia mtindo huu, atagundua kuwa afikapo mwisho wa usomaji wa riwaya, tamthilia au hadithi fupi, atakuwa na zaidi ya maswali 100 ya muktadha.

Mwalimu ampe kiranja au mwanafunzi yeyote jukumu la kumsaidia kunukuu majibu kwa maswali hayo kisha ayachapishe.

Mbinu hii itamrahisishia mwalimu mambo mengi, hivi kwamba atakuwa na mifano mingi ya maswali na majibu kwa ajili ya marudio.

You can share this post!

Wakenya wachemka kupinga ada ya ujenzi wa nyumba

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kukua na kuenea kwa Kiswahili...

adminleo