Ajax yaipepeta Juventus, yatinga nusu-fainali Klabu Bingwa Barani Ulaya
Na MASHIRIKA
TURIN, Italia
Hata baada ya kupuuzwa kwa kiasi kikubwa Jumanne usiku, vijana Ajax Amsterdam walitoka nyuma na kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Juventus na kufuzu kwa nusu-fainali ya michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA).
Hii ilikuwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22 kwa klabu hiyo ya Uholanzi kutinga hatua hiyo. Timu hizo zilitoka sare 1-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza jijini Amsterdam, na sasa Ajax wamefuzu kwa jumla ya mabao 3-2.
Cristiano Ronaldo aliwapa matumaini mashabiki wa nyumbani alipofunga bao dakika ya 28, likiwa lake la 126 katika mashindano hayo ya Ulaya, kabla ya mlinzi Donny van de Beek kusawazisha dakika sita baadaye.
Bao la kuzamisha jahazi la vigogo wa Turin lilimiminwa wavuni na nahodha Matthijs de Ligt ambaye kwa sasa anawindwa na timu kadhaa za ligi kubwa duniani.
Baada ya ushindi huo, Ajax wanasubiri Tottenham Hotspur walitoka na Manchester City kwa jumla ya mabao 4-4 baada ya mikondo miwili ila walikuwa ugenini wakijivunia ushindi wa 1-0 waliopata nyumbani. Sasa mabao yao matatu ya Jumatano usiku yakawasaidia sana licha ya City kufunga mabao manne.
Baada ya mechi yao dhidi ya Ajax, kocha wa Juventus Massimillian Allegri alisema: “Wapinzani wetu walitupa shida sana katika kipindi cha pili hasa baada ya kupata bao la pili. Kwa hakika walistahili kufuzu.”
Akaongeza: “Wengi walitarajia nijiuzulu, lakini siondoki kwa sababu hata Rais wa klabu, Andrea Agnelli anataka nibaki. Anataka tukae chini na kuzungumza kuhusu mustakabali wa timu hii.”
Ulikuwa ushindi mwingine mkubwa kwa vijana wa Ajax ambao hapo awali waliwabandua miamba Real Madrid.
Ajax walizima matumaini ya Ronaldo kutwaa ubingwa wa michuano hii kwa mara ya nne mfululizo, baada ya hapo awali kufanya hivyo mara tatu akiwa Real Madrid.
Vijana hao ambao katika kipindi cha pili waliumiliki mpira kwa kiasi kikubwa walitinga nusu-fainali kwa mara ya mwisho msimu wa 1996/97.
Juventus waliingia uwanjani bila beki wa kutegemewa, Giorgio Chiellini anayeuguza jeraha ambapo kukosekana kwake kulimfanya kipa Woyciech Szczesny kufanya kazi ya ziada kuokoa hatari nyingi langoni.
Juhudi za Ronaldo kufunga bao la kusawazisha mechi ikielekea kumalizika ziliambulia patupu alipozuiliwa na mabeki alipokuwa akijiandaa kuachilia kombora akiwa katika eneo la hatari.
Ushindi wa Ajax umepewa umuhimu kwenye vyombo vya habari nchini Uholanzi ambavyo vimedai ni ushindi wa kihistoria.
Magazeti yalitilia umuhimu habari hizo ni pamoja na De Telgraaf na De Volksrant lililosema: “Ajax imembandua mfalme wa soka ya Ulaya Ronaldo aliyesajiliwa na Juventus ili kuwashindia taji hilo.”
“Baada ya kubandua miamba wa Real Madrid na baadaye Juventus, kazi iliyobaki ni rahisi. Vijana wako tayari kuvuruga yeyote atakayekuja mbele yao na kufuzu kwa fainali. Awe Tottenham au Manchester City,” magazeti yote nchini humo yaliandika.