• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KICHAPO: Solkjaer akiri kikosi chake chahitaji mageuzi kufuatia kichapo cha Barcelona

KICHAPO: Solkjaer akiri kikosi chake chahitaji mageuzi kufuatia kichapo cha Barcelona

Na MASHIRIKA

BARCELONA, Uhispania

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United amekiri kwamba kikosi chake kinahitaji mabadiliko makubwa baada kuadhibiwa vikali na Barcelona katika mechi ya kufuzu kwa nusu-fainali ya Klabu Bingwa Barani Ulaya, Jumanne usiku.

Baada ya kichapo cha 1-0 katika mkondo wa kwanza ya robo-fainali ugani Old Trafford, Manchester United walipokea kichapo kingine cha 3-0 katika pambano la marudiano ugenini ugani Camp Nou.

Barcelona walipata mabao yao kupitia kwa staa Lionel Messi aliyefunga mawili huku jingine likipatikana kupitia kwa Philippe Countinho.

Messi alitangulia kuona lango dakika ya 16 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 20.

Kocha Ole Gunnar Solskjær wa Manchester United. Picha/ Maktaba

Countinho alifunga katika dakika ya 61.

“Ni matokeo ya kushangaza ambayo yametubidi tuzungmze na wachezaji kuwaambia wajitahidi zaidi, wakati huu tunapanga kutimua baadhi yao. Tuna wachezaji wengi na tumepiga hatua nzuri kwa kufika robo-fainali, lakini sasa kilichobakia ni kuwania nafasi ya kumaliza miongoni mwa nne bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Hata hivyo, tumewaambia ni lazima timu ijengwe upya. Nimewahi kusema hapo awali kwamba kikosi cha sasa kinahitaji mabadiliko makubwa. Lakini mabadiliko hayo hayawezi kufanyika kwa siku moja. Ili tufikie kiwango cha Barcelona, lazima tukubali kuyafanya mabadiliko hayo.”

Messi alionyesha mchezo uliothibitisha kilichomfanya anyakue tuzo ya Ballon d’Or mara tano.

“Kwa hakika Messi ni moto wa kuotea mbali,” alisema Solkjaer.

“Yeye na Cristiano Ronaldo watazidi kusalia wachezaji bora duniani hadi watakapostaafu. Usiku wa leo (Jumanne) ameonyesha uwezo wake na mchango wake mkubwa kikosini. Kila alipopata mpira karibu na eneo alituchanganya na kutoa pasi ambazo zilimfanya kuwa mchezaji aliyetamba zaidi.”

Kocha, Ernesto Valverde alikubaliana na maoni ya Solskjaer kwamba Messi aling’ara kuliko wote usiku huo.

“Tulipokuwa Old Trafford hakucheza vizuri kwa sababu alikuwa akiuguza jeraha, lakini ameonyesha umahiri wake katika mechi ya leo usiku (Jumanne) na kila mtu ameshuhudia hadharani,” alisema Valverde.

“Hata baada ya kuumizwa puani na Chris Smalling, Messi alidhihirisha uhodari wake kwa kufunga mabao mawili kwa kishindo. Kufunga mabao mawili katika muda usiozidi dakika 20 kwenye mechi kubwa sio rahisi.”

Ushindi huo umeiwezesha Barcelona kutinga nusu-fainali kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa miaka minne.

Vyombo vya habari jijini hapa vimemsifu Messi vikisema ndiye hodari zaidi kwa sasa, baada ya dunia kukosa mchezaji wa kiwango hicho kwa muda mrefu.

Kufikia sasa, Messi ambaye ni mshindi wa mchezaji bora Uropa, mshindi mara tano wa tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa, ameifungia Barcelona mabao 597.

Hata hivyo, sio tu kwa sababu ya kufunga mabao, bali vitu anavyofanya akiwa uwanjani. Mchango wake kikosini umekuwa mkubwa zaidi.

Kabla ya ushindi wa Jumanne, Barcelona walikuwa hawajapita hatua ya robo-fainali, tangu wabanduliwe na Atletico, Juventus na Roma.

You can share this post!

Ajax yaipepeta Juventus, yatinga nusu-fainali Klabu Bingwa...

SHANGAZI AKUJIBU: Ninampenda ajabu lakini naye amezidi kwa...

adminleo