Thamani ya shilingi ya Kenya yazidi kushuka
Na BERNARDINE MUTANU
Shilingi ya Kenya inazidi kudhoofika dhidi ya dola, kwa miezi mitatu mfululizo thamani yake inazidi kushuka.
Kutokana na hilo, huenda mfumuko wa bei ya bidhaa ukaanza kushuhudiwa nchini.
Kutokana na hilo, huenda gharama ya maisha ikazidi kuongezeka huku mamilioni ya wananchi wakizidi kuathiriwa na njaa.
Kiwango cha mfumuko wa bei ya bidhaa ni asilimia 4.35 kutoka asilimia 4.14 mwezi wa Machi kutokana na ongezeko la bei ya chakula.
Kulingana na wafanyabiashara, kudhoofika kwa shilingi kumetokana na dhamana za serikali zinazoendelea kukomaa.
“Shilingi ya Kenya ilidhoofika dhidi ya dola Jumatano kwa sababu ya ongezeko la pesa sokoni na mahitaji mengi ya dola na waagizaji wa bidhaa kutoka nje,” alisema mfanyabiashara kama alivyonukuliwa na Reuters.
Kufikia saa tisa kasoro dakika 20, sarafu ya Kenya ilikuwa ikibadilishana na dola ya Marekani kwa 101.30, thamani ya chini zaidi tangu Januari 24 ilipokuwa 101.41 dhidi ya dola.
Thamani ya juu zaidi ya shilingi dhidi ya dola ilikuwa ni 99.61 mnamo Machi 12 na kufikia sasa imeshuka kwa asilimia 1.7 tangu wakati huo.
Lakini bado sarafu hiyo ni dhabiti zaidi ikilinganishwa na mwanzoni mwa mwaka ambapo ilikuwa ni 101.83 dhidi ya dola.