AFYA NA USAFI: Matumizi ya baking powder na baking soda nyumbani mbali na uokaji
Na MARGARET MAINA
BAKING powder inayopatikana jikoni na ambayo hutumika sana katika uokaji wa vyakula kama keki, mikate, maandazi na vyakula vingine, pia hutumika kulainisha vyakula ambavyo ni vigumu kuiva kama mahindi na mboga za kienyeji.
Mbali na matumizi hayo, baking powder pia unaweza kutumika jinsi ifuatavyo:
Kusafisha kibao cha kukatia nyama au mboga
Kibao cha kukatia mara mingi hushika uchafu na hata kubadilika rangi, hata baada ya kukiosha. Kutatua tatizo hilo na kufanya kibao chako kiwe safi na cheupe tena, nyunyuzia baking soda ya kutosha katika kibao kisha sugua.
Kama ni uchafu wa muda mrefu kilowe kibao kwa maji kisha nyunyuzia baking soda na uache kwa dakika 15 kisha usugue.
Kuzibua sinki jikoni
Sinki la jikoni mara nyingi huziba kupitisha maji machafu kwa sababu ya mafuta na uchafu wa chakula.
Mwagilia kikombe kimoja cha baking soda kwenye sinki, kisha mwagia maji ya moto.
Kuondoa harufu chooni
Chukua nusu kikombe cha baking soda changanya na nusu kikombe cha vinegar nyeupe kisha mwaga ndani ya choo na unyunyuzie kwenye sakafu.
Iwache kwa muda ya nusu saa kisha piga deki sakafu.
Kusafisha ovena
Unapooka vyakula kama nyama, samaki au mboga za majani umajimaji kutoka kwenye vyakula hivi humwagika ndani ya ovena. Wakati mwingine unapotengeneza mchuzi, mafuta huruka na kuchafua ovena.
Ili kusafisha, weka baking soda ya kutosha kwenye sehemu ya chini kabisa ya ovena, kisha iloanishe na maji kiasi. Iache kwa muda kabla ya kusafisha.
Kuondoa harufu mbaya ndani ya jokovu
Kutokana na uwekaji wa vyakula vya aina mbalimbali vyenye harufu tofauti tofauti, mara nyingi jokovu huwa na harufu.
Ifungue baking soda kisha iweke kwenye sehemu ya chini ya friji yako liwache kwa muda hadi harufu utakapokwisha.
Mbali na matumizi hayo magadi soda pia husaidia kung’arisha meno, kusafisha kucha na hata kuondoa chunusi usoni.