• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
USAFI: Bidco Africa yapiga jeki shule

USAFI: Bidco Africa yapiga jeki shule

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Bidco Africa Ltd imejitolea kuona ya kwamba inasambaza vifaa na bidhaa muhimu wakati wa kunawa mikono miongoni mwa wananchi na katika shule.

Mnamo Alhamisi kampuni hiyo ilizuru shule ya upili ya State House Girls’ ya Nairobi na kusambaza bidhaa ya Gental care hand washing kwa minajili ya kunawa mikono kila mara.

Kwa mujibu wa afisa wa mawasiliano Bw John Lawrence, lengo lao lilikuwa kuwahamasisha walimu na wanafunzi kunawa mikono kila mara kwa sababu bado homa ya corona ingalipo.

“Tutaendelea kuzuru shule kadha za humu nchini kwa lengo la kusambaza bidhaa zetu na kuwahamasisha walimu na wanafunzi umuhimu wa kujiweka chonjo,” alisema Bw John Lawrence.

Alisema hatua hiyo ikifuatiliwa kwa makini bila shaka “tutakuwa tumepiga hatua zaidi kwa kukabiliana na janga la corona.”

Alisema kampuni ya Bidco Africa itafanya juhudi kuzuru makazi ya wananchi jijini Nairobi na Kiambu ili kuwahamasisha jinsi ya kunawa mikono na kuchukulia jambo hilo kwa uzito.

“Ingawa ni jambo linaloonekana kuwa rahisi kufanya, lakini ni muhimu liwe kama uraibu wa kila mara ili kusaidia kukabiliana na janga la corona,” alisema.

 

Walimu wa shule ya upili ya State House Girls wakihamasishwa kuhusu umuhimu wa kunawa mikono na afisa wa mawasiliano wa Bidco Africa Ltd Bw John Lawrence (wa pili kushoto) aliyesimama. Picha/ Lawrence Ongaro

Mwalimu mkuu wa State House Girls’ Bi Everlyne Nabukhwesi, alisema kwa sababu shule zimefunguliwa, litakuwa jambo la busara kutilia mkazo kunawa mikono kila mara.

“Wakati huu kunawa mikono kutakuwa ni kama sheria na mambo hayatakuwa kama hapo awali. Wakati huu kila mara tutalazimika kufuata wito,” alisema Bi Nabukhwesi.

Kulingana mpangilio wa shule hiyo, kuna vituo 45 vya kunawa mikono ambapo hiyo ni mojawapo ya hatua zilizochukuliwa na shule hiyo.

Siku chache zilizopita kampuni hiyo pia alizuru shule ya walemavu ya Thika School for the Blind.

Afisa wa bidhaa za matumizi za nyumbani Bi Anne Muiruri alisema lengo lao kuu ilikuwa kuona ya kwamba wanafunzi walio na ulemavu wa macho pia wanapata nafasi ya kutumia bidhaa za Bidco.

“Tutaendelea kusambaza bidhaa zetu bila ubaguzi wowote nchini kwa lengo la kuona ya kwamba tunatumikia kila mwananchi popote alipo,” alisema Bi Muiruri.

Alisema shule zitakapofunguliwa kikamilifu hivi karibuni, kampuni hiyo itazuru shule nyingi zaidi ili kutekeleza lengo lake la kuhamasisha kila mmoja umuhimu wa kunawa mikono na kudumisha usafi.

You can share this post!

Kivumbi chaanza Joho akitua Msambweni

Aliyechoma mwili wa mpenziwe motoni