Mama adaiwa kushirikiana na wanawe kuua mumewe
NDUNGU GACHANE na GEORGE MUNENE
POLISI katika Kaunti ya Murang’a wanamzulia mwanamke na wanawe watatu kwa madai ya kushirikiana kumuua mumewe.
Wanachunguza madai kuwa mwanamke huyo aliuteketeza mwili wa mume huyo na akajaribu kuuzika katika shimo alilochimba nje ya nyumba yao kufuatia mzozo wa kinyumbani.
Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa kumi na moja alfajiri kuamkia jana, katika kijiji cha Good Samaritan eneo la Kakuzi, eneo bunge la Gatanga.
Iiliripotiwa kuwa wawili hao wamekuwa na mizozo ya kinyumbani iliyomfanya mwanamke huyo kumpiga mumewe kwa nyundo hadi akafa kabla kumkata kwa upanga na shoka.
Kisha alizitupa silaha hizo ndani ya shimo la choo, akaburuta mwili wa marehemu nje ya nyumba na kuuteketeza akitumia godoro.
Mkuu wa Polisi Kaunti ya Murang’a, Bw Josphat Kinyua, alithibitisha kisa hicho na kusema mwanamke huyo pamoja na wanawe wamekamatwa na uchunguzi kuanza. Alisema polisi walipokea habari kutoka kwa wanakijiji.
“Tumemkamata mshukiwa na watoto wake watatu wanaodaiwa kumuua baba yao. Nahimiza wanandoa kusaka mbinu mwafaka za kisheria kusuluhisha mizozo yao ya ndoa badala ya kuangamizana,” alieleza Bw Kinyua.
Majirani walioshuhudia kisa hicho waliambia Taifa Jumapili kwamba, mwili wa John Maina ulikuwa na majeraha ya moto na mengine. Majirani hao waliojumuisha ndugu ya marehemu James Ndirangu walisema kuwa walivutiwa na moto mkubwa katika boma hilo.
Katika kaunti ya Kirinyaga, karani wa korti, Stanley Mureithi Muriuki, 45, aliuawa na wakazi kwa kuchomwa alipokataa mwanawe wa kiume azikwe kwenye shamba la familia.
Wakazi wa kijiji cha Gitumbi pia waliharibu mali ya maelfu walipoichoma nyumba yake.
Kijana wa karani huyo aliyetambuliwa kwa jina la Kelly, 18, alikuwa amejiua kwa sababu ambazo polisi wanachunguza. Bw Muriuki ambae hufanya kazi katika mahakama ya Murang’a alianza kuwatusi wakazi waliokuwa wakiandaa mazishi ya mwanawe katika shamba lake.