Habari Mseto

Wawili hawajulikani waliko baada ya boti kuzama

April 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

MABAHARIA wawili hawajulikani waliko ilhali wengine wawili wakiokolewa pale mashua waliyokuwa wakisafiria ilipozama karibu na kivuko cha Manda Bruno, Kaunti ya Lamu Jumapili.

Akithibitisha ajali hiyo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri, alisema mashua hiyo inaaminika ilizama kufuatia kubeba mizigo kupita kiasi.

Bw Kanyiri alisema maafisa wa polisi wa marini wakishirikiana na maafisa wa Bodi ya Udhibiti wa vyombo vya baharini (KMA) na wapigambizi wa kujitolea tayari wamepiga kambi kwenye eneo la ajali kutafuta wale walipotea baharini.

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa nne asubuhi saa machache baada ya mashua kuondoka kwenye jeti ya Mokowe ikiwa imebeba mawe na kokoto hizo za ujenzi kuelekea kisiwa cha Pate.

“Ni kweli. Kumekuwa na ajali ambapo mashua iliyobeba vifaa vya ujenzi, ikiwemo mawe na kokoto ilipozama karibu na kivuko cha Manda Bruno. Mashua yenyewe ilikuwa na mabaharia wanne. Wawili kati yao wameokolewa ilhali wengine wawili wakiwa hawajulikani waliko. Juhudiu za kuwatafuta waliopotea zinaendelea kwa sasa kwenye eneo la tukio,” akasema Bw Kanyiri. Aliwatahadharisha mabaharia dhidi ya kubeba mizigo kupita kiasi na kuendesha boti na mashua zao kwa mwendo wa kasi.

Bw Kanyiri pia aliwataka mabaharia kuwa waangalifu wakati huu ambapo msimu wa upepo mkali na mawimbi baharini unaanza.

“Ninavyofahamu ni kwamba msimu wa dhoruba kali na mawimbi baharini umewadia. Ningewasihi mabaharia kujua vyema hali ya bahari ili kuepuka maafa,” akasema Bw Kanyiri.

Ajali za boti zinazosababisha watu kupotea baharini na hata maafa si ngeni kaunti ya Lamu.

Mnamo Agosti, 2018, wavuvi watatu waliripotiwa kupotea baada ya mashua yao kuzama eneo la Ndau kaunti ya Lamu.

Watatu hao bado hawajapatikana hadi sasa.

Mnamo Juni, 2018, wavuvi wawili walifariki ilhali wengine watatu wakiokolewa pale mashua waliyokuwa wakitumia kuvulia iliposombwa na mawimbi makali na kuzama baharini eneo la Manda-Maweni, Kuanti ya Lamu.

Mnamo Agosti 13, 2017, watu 12 wakiwemo watoto, bibi na shangazi wa mwanasiasa wa ODM, Bw Shekuwe Kahale, walifariki pale boti walimokuwa wakisafiria kutoka Kizingitini kuelekea kisiwa cha Lamu kuzidiwa na mawimbi makali na kuzama baharini katika eneo la Manda Bruno.

Juni 20, 2017, watu 10 walifariki papo hapo pale mashua walimokuwa wakisafiria kutoka kisiwa cha Lamu kuelekea Ndau ilipozama baharini katika eneo la kivuko cha Mkanda.