• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Polisi wazidisha doria Salgaa kuepusha ajali

Polisi wazidisha doria Salgaa kuepusha ajali

Na KEVIN ROTICH

MSHIRIKISHI wa Serikali eneo la Bonde la Ufa, Mongo Chimwaga, amewataka madereva kuwa waangalifu wanapoendesha magari kwenye barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Eldoret msimu huu wa sherehe za Pasaka.

Afisa huyo wa utawala pia alisema wameongeza maafisa kadhaa wa polisi kwenye barabara hiyo yenye shughuli nyingi ili kuhakikisha sheria za trafiki zinazingatiwa kuzuia ajali na vifo.

“Maafisa wa polisi wamezidisha doria kwenye barabara ya Nairobi-Nakuru-Eldoret. Nawaomba madereva na watumizi wa barabara wazingatie sheria za trafiki msimu huu wa Pasaka. Tunatarajia wengi watakuwa wakirejea kazini leo na kesho na tunawaomba wazingatie nidhamu kwenye barabara hii,” akasema Bw Chimwaga.

Iliripotiwa kwamba mtu mmoja alifariki na mwingine kujeruhiwa vibaya kwenye ajali katika daraja la Salgaa, barabara ya Nakuru-Eldoret. Msafiri aliyejeruhiwa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Molo huku mwili wa mwendazake ukihifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Nakuru.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Rongai, Richard Rotich alisema ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa mbili asubuhi, ilihusisha trela na Lori.

“Mwendeshaji wa trela lililokuwa likielekea Eldoret alikuwa upande usiofaa barabarani ndipo akagongana na lori lililokuwa likielekea Nakuru. Naomba madereva wawe makini kwa kuwa barabara hii ina historia mbaya ya ajali,” akasema Bw Rotich.

Kulingana na mkazi Tito Wanyama, ajali nyingi zilizoishia vifo na majeraha zimetokea katika daraja la Salgaa. “Haupiti mwezi moja kabla ajali kutokea,” akasema Bw Wanyama.

Barabara ya Nairobi-Nakuru-Eldoret imekuwa ikigonga vichwa vya habari kutokana na ajali nyingi hasa katika daraja la Salgaa ambalo kutajwa kwake kunawahofisha wasafiri.

Maeneo mengine yenye historia ya ajali mbaya ni Kikopey, Sobea, Salgaa, Migaa, Sachangwan na Mau Summit.

You can share this post!

Magavana 10 Mlima Kenya waanza kujitenga na Ruto

Mama Sarah Obama kuadhimisha umri wa miaka 97

adminleo