Habari MsetoSiasa

Mchakato wa kumkagua Mhasibu Mkuu waanza

April 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

BUNGE limeanzisha tena mchakato wa kutafuta mkaguzi atakayemchunguza Mhasibu Mkuu wa Hesabu za serikali Edward Ouko.

Kampuni itakayochaguliwa itachunguza vitabu vya uhasibu vya Bw Ouko ambavyo havikuchunguzwa kwa miaka ya kifedha ya 2014/2015, 2015/2016, 2016/2017 na 2017/2018.

Hatua hiyo ni kwa mujibu wa Katiba Kifungu cha 226(4) cha Katiba ambacho kimependekeza Bunge la Kitaifa kuteua wahasibu kuhasibu afisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali.

Kufuatia hilo, Bunge la Kitaifa lilizitaka kampuni zilizohitinisha mahitaji kutuma maombi ya kutoa huduma ya kuhasibu afisi hiyo kwa kipindi cha miaka minne ambayo haikuchunguzwa.

“Kutakuwa na mkutano kabla ya kutuma maombi kwa kampuni zote zinazotaka kutoa huduma hiyo Jumatano Aprili 17 saa tano asubuhi,” alisema Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai katika tangazo la gazeti.

Bunge litafungua mapendekezo Jumatano Aprili 24, 2019 mbele ya wote waliotuma maombi ambao pia wanaweza kutuma wawakilishi wao.

Hii ni mara ya nne Bunge la Kitaifa linalenga kuajiri mkaguzi kuhasibu vitabu vya uhasibu vya Bw Ouko.

Bw Ouko anatarajiwa kuondoka afisini Agosti mwaka huu bila kukaguliwa na mkaguzi wa kibinafsi pamoja na Bunge.

Mnamo Februari, Bw Sialai na Kamati ya Hesabu za Umma (PAC) aliidhinisha kutafuta huduma za kampuni ya kimataifa kukagua vitabu vya Mhasibu Mkuu wa Serikali baada ya jaribio hilo kufeli mara tatu.