• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
KAULI YA MATUNDURA: Mchango wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Fasihi Tafsiri ya Kiswahili

KAULI YA MATUNDURA: Mchango wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Fasihi Tafsiri ya Kiswahili

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO Oktoba 2007 mtaalamu wa sheria na mwanaharakati Prof Issa Shivji alihojiwa na gazeti la “Mwananchi” la Tanzania.

Mahojiano hayo yalihusu maadhimisho ya miaka minane tangu kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Swali la kwanza aliloulizwa mwanataaluma huyu lilihusu maoni yake kuhusu Tanzania bila Nyerere.

Prof Shivji alisema, pamoja na kwamba Tanzania ilikuwa na watu ambao wangeweza kujaza pengo la uongozi lililoachwa na Mwalimu Nyerere, hayati alikuwa na upekee wa namna yake – ukiwemo udumishaji wa utamaduni na kipawa cha kuona mbali.

Alidai kwamba Tanzania bila Mwalimu ilikosa sauti ya kuonya, kutahadharisha , kutegemea, kuongoza na kuchochea fikra – hata kwa wengi waliokuwa hawakubaliani naye.

Katika makala haya, ninatathmini ‘ualimu’ wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika maendeleo ya Kiswahili kwa jumla – na hasa taaluma ya tafsiri.

Lakabu ya ‘mwalimu’ ilishika na kuwa sehemu ya jina la Rais Nyerere kwa sababu kitaaluma, alikuwa mwalimu katika shule za upili za Tabora na Pugu.

Fasiri ya kileksika ya ‘mwalimu’ ni mtu afundishaye elimu au maarifa fulani; mtu anayesomesha wengine. Hata hivyo, tunaweza kuipanua maana ya neno ‘mwalimu’ kama kiongozi, mtumishi kwa watu wengine na mwanafalsafa.

Makala haya mafupi yanajikita katika muktadha wa ‘ualimu’ na tafsiri kwa Kiswahili za kazi za mwandishi wa Uingereza – William Shakespeare (1564 – 1616).

Mwalimu Julius Nyerere alitafsiri tamthilia mbili za mtunzi huyu kutoka kwa Kiingereza hadi Kiswahili.

Kazi hizi ni pamoja na Julius Caesar kama Juliasi Kaizari (Oxford University Press, 1968) na ‘The Merchant of Venice‘ kama ‘Mabebari wa Venisi’ (Oxford University Press, 1969).

Adhihirisha ualimu

Katika kuivalia njuga taaluma ya tafsiri, Mwalimu Nyerere alidhihirisha ‘ualimu’ wake na hivyo basi kutufundisha mawili.

Kwanza, Mwalimu Nyerere hakuzitafsiri tungo za Shakespeare kutoka kwa Kiingereza hadi Kiswahili kwa sababu ya kukipenda Kiingereza – bali alikipenda Kiswahili zaidi.

Pili, hatua ya kujishughulisha na tafsiri ilikuwa ya kijasiri mno ili kutaka kuonesha kwamba lugha ya Kiswahili ina uwezo wa kusheheni maarifa ya staarabu nyingine ulimwenguni.

Tunapaswa kukumbuka kwamba tamthilia mbili za William Shakespeare ambazo nimezitaja zimeandikwa kwa muundo wa kishairi.

Mwalimu Nyerere amafaulu kwa kiasi kikubwa kudumisha mtindo huo kwa kutumia ushairi wa Kiswahili kadri ya uwezo wake.

Hali hii ilisababisha Mwalimu Nyerere kukumbana na matatizo mengi katika kutafsiri tungo za Shakespeare kwa Kiswahili.
Julius Kambarage Nyerere – mbali na kuwa rais wa Tanzania alikuwa mwanafalsafa.

Tunaweza kuona jinsi mawazo kuhusu falsafa ya Ujamaa wa Kiafrika yalifanikiwa pakubwa katika kuunganisha zaidi ya makabila 100 nchini Tanzania – licha kwamba mwelekeo huo ulimaskinisha taifa hilo.

Mawazo na mwonoulimwengu wa Mwalimu Nyerere bado vinazidi kuacha taathira ya namna fulani miaka mingi baada ya kifo chake.
Watu wa aina hiyo aghalabu hawahitaji kujengewa minara ya kumbukumbu. Tafsiri za Mwalimu Nyerere ni mnara na kumbukumbu ya kutosha tunapozungumzia maendeleo ya fasihi tafsiri ya Kiswahili.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

[email protected]

You can share this post!

Gathoni Wa Muchomba awakosoa viongozi ambao kila wakiamka...

Mfumo wa kutumia gilasi za plastiki kupanda miche, je, zipo...

adminleo