• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
GWIJI WA WIKI: Geoffrey Omoga Matiabe

GWIJI WA WIKI: Geoffrey Omoga Matiabe

Na CHRIS ADUNGO

KISWAHILI kina uwezo wa kukutoa hapa na kukuweka hapo kabla ya kukufikisha pale.

Kuna idadi kubwa ya watu ambao kwa sasa wanajivunia mafao ya Kiswahili ulimwenguni.

Siri ya mafanikio yao imekuwa ni kufuata misukumo ya ndani ya nafsi zao hadi ndoto zao zikatimia.

Kwa hivyo, lenga kuwa bora katika chochote unachoteua kukishughulikia. Kwa kuwa Mola ndiye mwelekezi wa hatua zote tunazozipiga maishani, inatujuzu kumweka mbele siku zote.

Kufaulu katika jambo lolote kunahitaji mtu kuwa na maono na kutenda mema bila ya kudhamiria malipo. Nidhamu, bidii na imani ni kati ya mambo mengine yanayochangia mafanikio ya binadamu.

Anza kushindana na wakati badala ya binadamu wenzako.

Jikubali jinsi ulivyo na uache kujilinganisha na watu wengine.

Kujilazimishia maisha ya mtu mwingine ambaye si wa kufu yako kutakufanya kuishi katika uoga. Matokeo yake ni kwamba utaanza kujidharau, kujisuta na kujihukumu.

Kataa kukataliwa na uondoe hofu ya kujiona mtu asiyefaa, asiyestahili kabisa kuishi au asiyeweza kufanya jambo lolote la maana.

Hakuna mtu hata mmoja asiye na uwezo wa kukufundisha kitu kipya.

Hata katika ujinga, kuna hekima. Hicho unachokipuuza ndicho wenzako wanakikeshea kwa matumaini kwamba kitawavusha hadi kiwango kingine cha juu zaidi maishani.

Huu ndio ushauri wa Bw Geoffrey Omoga Matiabe – kocha shupavu wa tenisi na mpira wa magongo ambaye kwa sasa ni mwalimu na Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Asumbi Girls, Kaunti ya Homa Bay.

Maisha ya awali

Mwalimu Matiabe alizaliwa mnamo 1976 katika kijiji cha Mokubo, eneo la Kenyenya, Kaunti ya Kisii akiwa mtoto wa tatu kati ya sita katika familia ya Bi Rudia Matiabe na marehemu Mzee Matiabe Matini.

Baada ya kupata elimu ya msingi katika Shule ya Magenche, Kenyenya kati ya 1981 na 1988, alijiunga na Shule ya Upili ya Riokindo, Kenyenya mnamo 1989.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 1992 baada ya kuibuka mwanafunzi bora shuleni Riokindo na hivyo kuendeleza ubabe aliokuwa ameudhihirisha tena katika mtihani wa KCPE.

Mbali na walimu waliomchochea kuandika insha bora zilizomzolea tuzo za haiba kubwa akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, Matiabe anatambua pia upekee wa mchango wa wazazi wake katika kumwelekeza vilivyo, kumtia katika mkondo wa nidhamu kali, kumhimiza na kumshajiisha zaidi kujitahidi masomoni.

Anakiri kwamba alivutiwa sana na watangazaji wa redio; hususan marehemu Billy Omalla ambaye zaidi ya ufahamisho wake, alimtandikia zulia zuri la Kiswahili na kumfundisha mengi kupitia kipindi alichokuwa akikiendesha katika Idhaa ya KBC, Maswali kwa Wanafunzi.

Matiabe alianza kupendezwa na taaluma ya utangazaji akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi kiasi cha kuchochewa kuziiga sauti za baadhi ya wanahabari kila walipokuwa wakitangaza taarifa na kuendesha vipindi redioni.

Usomi

Mnamo 1994, Matiabe alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili na Dini).

Anawaenzi mno wahadhiri waliofanikisha safari yake ya elimu chuoni, hasa Profesa John Habwe, Bw Karanja, Dkt Ayub Mukhwana na Profesa Rayya Timammy ambao mbali na kumpokeza malezi bora ya kiakademia, pia walimrithisha ilhamu na kariha ya kukichapukia Kiswahili.

Wengine waliomchochea zaidi kwa imani kwamba Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hiyo ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi, ni Dkt Zaja Omboga na Dkt Amiri Swaleh ambaye hadi leo, ni miongoni mwa marafiki wake wakubwa.

Matiabe alifuzu na kuhitimu mwishoni mwa 1998 ingawa hapo awali, kifo cha babake mzazi kilitishia kuuzima kabisa mshumaa wa tumaini lake la kukamilisha masomo ya chuo kikuu.

Msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ulimchochea kujiunga na Chuo Kikuu cha Kisii mnamo 2013 kusomea shahada ya Uzamili katika Filosofia ya Elimu.

Anatarajia kufuzu kufikia mwisho wa mwaka 2019.

Ualimu

Baada ya kuhitimu ualimu, alipata kibarua cha kufundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Orero, Kaunti ya Homa Bay mnamo 2000.

Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Asumbi Girls akiwa mwalimu aliyeajiriwa na Bodi ya Usimamizi (BOM awali ikiitwa BOG).

Ilikuwa hadi 2003 ambapo aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) katika Shule ya Upili ya Asumbi Girls.

Mnamo 2011, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili na Lugha Nyingine (isipokuwa Kiingereza). Huu ni wadhifa anaoushikilia hadi sasa.

Tangu 2013 Matiabe amekuwa mtahini wa kitaifa wa Karatasi ya Pili ya somo la Dini ya Kikristo (CRE) wa Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC).
Uzoefu huu pamoja na weledi wake katika Kiswahili umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini (zikiwemo Mirogi Boys na Kigoto High kutoka Homa Bay) kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Mwalimu Geoffrey Matiabe wa Asumbi Girls. Picha/ Chris Adungo

Ukocha

Mapenzi kwa michezo ya magongo na tenisi ni jambo lililoanza kujikuza ndani ya Matiabe tangu akiwa tineja.

Ingawa hivyo, Shule ya Upili ya Asumbi Girls ndiyo ilipanda zaidi na kuotesha mbegu za mapenzi ya dhati anayojivunia kwa sasa katika ulingo huo.

Umahiri wa vikosi vyake vya tenisi na hoki kutoka Asumbi Girls ni upekee ambao umekuwa ukimpandisha kwenye majukwaa mbalimbali ya mashindano ya haiba.

Kuanzia 2008 Asumbi Girls wamekuwa na uhakika wa kunogesha kampeni za kitaifa kwenye michezo ya tenisi, isipokuwa mwaka huu ambapo walibanduliwa katika hatua ya mchujo wakiwa miongoni mwa wawakilishi wa eneo la Nyanza.

Mnamo 2012 kikosi cha magongo kutoka Asumbi Girls kilifuzu kuwania ubingwa wa Michezo ya Afrika Mashariki miongoni mwa shule za upili na kikatia kibindoni nishani ya shaba.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, warembo hawa wamekuwa wakizidiwa maarifa na watani wao wa tangu jadi, Sinyolo Girls kutoka Kaunti ya Siaya.

Maazimio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake, Matiabe anapania kuwa mhadhiri wa Filosofia ya Elimu katika chuo kikuu.

Isitoshe, ana malengo ya kujitosa rasmi katika ulingo wa uandishi kwa imani kwamba safari yake katika sanaa ya utunzi ilianza tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi; akizibuni tungo zilizompokeza takrima za kila sampuli.

Jivunio

Mbali na kuwa mkulima mashuhuri wa miwa katika eneo la Trans-Mara, Matiabe anajivunia pia kuwa kiini cha motisha na hamasa ambayo kwa sasa inawatawala walimu wengi anaoshirikiana nao katika jitihada za kukitetea na kukipigania Kiswahili.

Anatambua mchango wa aliyekuwa mwalimu mwenzake shuleni Asumbi Girls, Bw Nandwa Omuhaka, katika kumwamshia ari ya kuuthamini Ushairi wa Kiswahili.

Bw Nandwa kwa sasa ni Naibu Mwalimu Mkuu katika shule mojawapo eneo la Vihiga na pia ni mwamuzi wa kupigiwa mfano katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Katika kipindi cha miaka 18 ya ualimu wake, Matiabe anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao wengi wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili. Mmoja wao ni Bi Phenny Awiti ambaye kwa sasa ni mwanaharakati wa haki za watu wenye Virusi vya Ukimwi (VVU).

You can share this post!

Wakazi wa Okwata walia ni zaidi ya miaka minane, zahanati...

Wabunge David Ochieng’, Mawathe waapishwa

adminleo