UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya Kiswahili katika ujenzi wa jamii mpya ya Afrika
Na CHRIS ADUNGO
LUGHA ni chombo muhimu sana cha mawasiliano kilichoundwa na sauti za nasibu za kusemwa na kutumiwa na jamii ya utamaduni fulani.
Jinsi ambavyo zipo jamii nyingi za tamaduni mbalimbali duniani, vivyo hivyo ziko lugha mbalimbali zilizoundwa kukidhi haja ya mawasiliano ya tamaduni mbalimbali.
Maingiliano ya jamii zenye tamaduni na lugha mbalimbali yanayotokana na mashirikiano katika shughuli za biashara na nyinginezo za kijamii, huzusha haja ya kuwepo kwa lugha moja itakayoweza kuwaunganisha watu hao wenye tamaduni na lugha mbalimbali.
Maingiliano kama hayo yanaweza kuwa katika viwango mbalimbali.
Kiwango cha kwanza ni kile cha mtu binafsi; ambapo mtu hutoka kwenye jamii yake na kwenda kuishi kwenye jamii inayozungumza lugha tofauti na ile ya kwao.
Katika hali kama hiyo, mtu huyo itabidi ajifunze lugha ya jamii ile ya pili ili aweze kuwasiliana nao.
Kiwango cha pili ni kile kinachohusisha mkusanyiko wa watu waliotoka kwenye tamaduni mbalimbali na hawana hata lugha moja ya kuwaunganisha.
Watu kama hawa wakikaa pamoja, huweza kuzusha lugha ya kati ambayo katika hatua za mwanzo itajulikana kama pijini na baadaye kama Krioli.
Kiwango cha tatu ni kile ambacho maingiliano ya watu wenye tamaduni na lugha mbalimbali husababisha kuteuliwa kwa lugha moja miongoni mwa lugha zao na kutumika kama chombo cha mawasiliano na cha kuziunganisha jamii zote husika.
Kiwango hiki chaweza kujitokeza katika ngazi ya wilaya, mkoa, nchi, kanda, bara na hata ulimwengu mzima.
Ukoloni
Katika enzi ya ukoloni katika Afrika Mashariki, haja ya kuwepo kwa lugha moja itakayotumika hususan katika elimu katika nchi zote za makoloni ya
Mwingereza wakati ule, yaani Tanganyika, Kenya, Uganda ilijitokeza.
Matokeo ya haja hii ni kuchaguliwa kwa Kiswahili, hususan lahaja ya Kiunguja itumike kama lugha ya kufundishia shuleni.
Vilevile, matokeo ya haja hiyo yalikuwa ni kuundwa kwa Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki mnamo mwaka 1925 na kuanza kazi mnamo 1930 iliyopewa mamlaka ya kuisanifisha lugha ya Kiswahili, ili kuwe na namna moja rasmi ya kusema na kuandika katika Afrika Mashariki.
Baada ya nchi za Afrika Mashariki kupata Uhuru, haja ya kuwepo kwa lugha moja kwa kila nchi kwa ajili ya mawasiliano na wananchi, na katika shughuli mbalimbali za kiserikali na za kijamii ikajitokeza.
Tanganyika ilipojipatia uhuru mwaka 1961 (Tanzania tangu 1964) ikajichagulia Kiswahili kilichokuwa kimekwishaenea nchi nzima kiwe Lugha ya Taifa na Kiingereza kiwe Lugha Rasmi katika masuala ya kiserikali na kimataifa.
Kenya ilipopata uhuru mnamo 1963 kwa kuwa haikuwa na lugha iliyokuwa imeenea nchi nzima, na kwa kuhofia mivutano ya kuchagua lugha moja ya wenyeji, haikuteua lugha ya taifa.
Hata hivyo, Kiingereza kiliteuliwa kuwa Lugha Rasmi katika masuala ya kitaifa na kimataifa.
Kiswahili ambacho kilikwishaanza kuongelewa na watu wengi, kilitumika katika kuwasiliana na wananchi katika mikutano ya siasa, biashara na kadhalika.
Uganda ilipata uhuru mnano 1962.
Ijapokuwa katika kipindi hicho lugha ya Luganda ilikuwa imekwishaenezwa nchini na watawala wa Kiganda, si Luganda wala lugha nyingine yoyote ya wenyeji iliyopteuliwa kuwa Lugha ya Taifa.
Whitely (1969), anadai kuwa “uteuzi wa watawala kutoka Buganda kutawala sehemu mbalimbali za Uganda, kulichangia kueneza lugha, lakini watawala hawa walionekana kama walikuwa wanapanua utawala wa Buganda, hivyo mwishowe lugha yao na wao wenyewe walichukiwa”.
Lugha nyingine ambayo ilikuwa imeenea kwa kiasi fulani nchini ilikuwa Kiswahili.
Ijapokuwa pendekezo la Gavana Sir W.F Gowers la kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya elimu na utawala na vilevile kuwa lugha ya mawasiliano (lingua franca) nchini kote lilipingwa vibaya na Kabaka Sir Daudi Chwa mnamo 1929, Kiswahili kiliendelea kupata mashiko.
Whitely (1969:70-71) anaripoti kuwa Kiswahili kiliendelea kutumiwa na polisi, sehemu za Kaskazini kuwasiliana na watu ambao hawajui Kiingereza na Luganda.
Vilevile wanilotiki wa Uganda walitumia sana Kiswahili kuwasiliana na makabila mengine.
Kiswahili kilitumika pia kwenye mipira, na sehemu nyingine ambazo lugha za Kiingereza na Luganda hazikuhitajika au hazikuwezekana kutumika.
Uteuzi
Hata hivyo, ili kukidhi haja ya mawasiliano, baada ya uhuru, Kiingereza kiliteuliwa kuwa Lugha Rasmi katika masuala ya kitaifa na kimataifa. Matumizi ya Kiswahili nchini Uganda yalishika kasi baada ya kuondolewa madarakani kwa Idd Amina Dada na kuingia madarakani kwa Rais Yoweri Museveni ambaye aliishi Tanzania kwa miaka kadhaa na elimu yake ya Chuo Kikuu kuipatia huko.
Katika bara la Afrika kwa ujumla, uundwaji wa ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi huru, pamoja na mambo mengine, ulizingatia kigezo cha lugha ya mawasiliano.
Kihistoria, ushirikiano baina ya Waafrika ulianza kabla nchi za Afrika hazijapata uhuru kati ya 1920-1957 chini ya dhana ya Upanafrika.
Lengo kuu lilikuwa kuzikomboa nchi hizo zitoke kwenye utawala wa kikoloni.
Ushirikiano baina ya nchi huru za Kiafrika ulianza baada ya nchi za Afrika kuanza kupata uhuru kati ya mwaka wa 1957 na 1960.
Malengo makuu ya awali ya ushirikiano yalikuwa kwanza, ni kupigania uhuru wa makoloni yaliyobaki na pili, kuunda muungano wa kisiasa wa bara zima chini ya serikali moja ya shirikisho.
Baada ya nchi nyingi za Kiafrika kujipatia uhuru kuanzia mwaka 1960, mgawanyiko ukaanza kujitokeza na wazo la kuwa na muungano wa kisiasa likaanza kufifia. Badala ya kufikiria muungano wa nchi zote za Afrika, makundi mbalimbali yakaanza kujitokeza.
Kwa mfano mwaka 1961, Ghana, Guinea, Egypt, Mali, Morocco, Libya na Algeria wakaunda kundi la Casablanka, makoloni yaliyobaki ya Wafaransa pamoja na Nigeria, Ethiopia, Liberia, na Siera Leone wakaunda kundi la Monrovia.
Mgawanyiko huu ulivunjwa makali yake baada ya Kwame Nkurumah, Sekou Tome na Modibo Keita wakiungwa mkono na Mfalme Haile Selassie kuitisha mkutano wa kilele wa Nchi huru za Kiafrika Mei 1963 na kuunda Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) mnamo Mei 25, 1963 (Asante, 2002).
Baada ya kuanguka kwa wazo la kuwa na muungano wa kisiasa wa bara lote, wazo la kuwa na vyombo vya kujikomboa kutokana na utegemezi wa kiuchumi lilijitokeza.
Wazo hili lilisababisha kuundwa kwa vyombo vya kiuchumi vya kikanda ambapo vikundi viliundwa kwa misingi ya lugha za mawasiliano.
Kwa upande wa nchi zinazozungumza Kiingereza, hapakuwepo na jumuiya za kiuchumi za kikanda zilizoundwa katika miaka ya mwanzo ya uhuru isipokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyoanzishwa na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mnamo Juni 1967.
Muungano huu ambao uliendesha mambo mengi kikanda kama vile biashara ya nje, sera ya fedha, miundo-mbinu ya usafiri na mawasiliano, na elimu haukudumu na ulivunjika Julai 1977.
Wakati wa Shirikisho la Afiika Mashariki, lugha iliyokuwa ikitumika wakati huo ilikuwa ni Kiingereza.
Haja ya kuwepo kwa Kiswahili haikujitokeza sana kwa sababu ushirikiano huu ulikuwa unatekelezwa na asasi za juu husika za Kitaifa na zile za Afrika Mashariki zilizoundwa chini ya ushirikiano huu. Kwa mfimo Bunge la Afiika Mashariki, Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Shirika la Reli la Afrika Mashariki, Shirika la Ndege la Afrika Mashariki, Makao Makuu ya Afrika Mashariki na kadhalika.
Haja ya kutumia Kiswahili haikujitokeza kwa vile, vyombo vilivyokuwa vinaendesha shirikisho hili vilikuwa vinaendeshwa na wasomi wanaoelewa Kiingereza.