• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
Waboni 3,000 waonja utamu wa hati miliki

Waboni 3,000 waonja utamu wa hati miliki

NA KALUME KAZUNGU

JUMLA ya Waboni 3,232 kwa mara ya kwanza wamepata hatimiliki za ardhi zao miaka 56 baada ya uhuru wa nchi hii kupatikana.

Hatimiliki hizo ni miongoni mwa zile 6,232 ambazo serikali ya kaunti ya Lamu ilikabidhi wakazi wiki hii.

Wakizungumza baada ya kupokea hatimiliki hizo jana, wakazi wa jamii ya Waboni waliitaja hatua hiyo kuwa mwamko mpya kwa jamii yao ambayo imekuwa ikitelekezwa na hata kutengwa kimaendeleo na haki kwa muda mrefu.

Waboni wanatambulika sana kwa maisha yao ya kutegemea msitu, ambapo wao kitega uchumi chao ni kuwinda wanyama pori, kuchuma matunda ya mwituni na kuvuna asali msituni.

Kwa miaka mingi, wakazi wa jamii hiyo wamekuwa wakiishi bila ya hati ya kumiliki ardhi zao, hatua ambayo ilikuwa ikichochea mabwanyenye na wanyakuzi wa ardhi kunyemelea ardhi hizo.

Waboni sasa wanasema kupatikana kwa hatimiliki za ardhi zao kutawawezesha kuzitunza vyema ardhi hizo na kuzilinda kutoka kwa wanyakuzi.

“Baadhi ya ardhi zetu zinapakana na mradi wa bandari ya Lamu (LAPSSET) na hii ndiyo sababu wanyakuzi wa ardhi wamekuwa wakinyemelea ardhi zetu kwa wingi. Natoa shukrani za dhati kwa serikali yetu ya kaunti na ile ya kitaifa kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha wakazi wa Lamu, ikiwemo Waboni wanapata hatimiliki. Huu ni mwanzo mpya na wa kihistoria kwetu,” akasema Bw Ali Gubo.

Mmoja wa wazee wa jamii ya Waboni, Bw Doza Diza alisema ni jambo la kufurahisha kwamba jamii hiyo pia imetambulika na kupewa haki ya kumiliki ardhi kama wakenya wengine nchini.

Bw Doza aliwashauri Waboni wengine kuepuka kuuza ardhi zao kiholela hasa baada ya kupokea hatimiliki za ardhi husika.

“Tunafurahia kuwa Wakenya pia. Tulikuwa tumebaguliwa tangu mwanzo lakini angalau kwa sasa tunajivunia kuwa wakenya. Ningewasihi Waboni wenzangu kuepuka kuuza ardhi zao kiholela,” akasema Bw Doza.

Kwa upande wake, Bi Asli Madobe alisema kupatikana kwa hatimiliki za ardhi kwa jamii ya Waboni kutasaidia pakubwa maendeleo kuafikiwa miongoni mwa jamii hiyo.

You can share this post!

Sonko na Sakaja wakabana koo

Mabapa mapya kuipa serikali Sh9 bilioni

adminleo