Habari MsetoSiasa

KANU na Jubilee, nani jogoo uchaguzi mdogo Wajir?

April 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GRACE GITAU na JOSEPH WANGUI

VYAMA vya KANU na Jubilee vinatarajiwa kupambana katika uchaguzi mdogo wa ubunge unaofanyika Alhamisi eneo la Wajir Magharibi.

Ibrahim Mohammed (KANU) na Ahmed Kolosh (Jubilee), ndio wanaong’ang’ania kushinda kiti hicho.

Baadhi ya watu wamechukulia uchaguzi huo kama vita vya ubabe baina ya fahali wawili wa Bonde la Ufa ambao ni Seneta wa Baringo, Gideon Moi na Naibu Rais William Ruto.

Uchaguzi huo umefanywa baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali uchaguzi wa Bw Kolosh, ambaye alikuwa amechaguliwa kwa chama cha ODM mnamo 2017.

Hata hivyo, Dkt Ruto alimpokea Kolosh alipohama kutoka ODM. Naibu Rais pia amehusishwa na kujiondoa kwa wagomeaji wengine wa kiti hicho ambao ni Mohamed Elmy, Ali Noor Abdi na Abass Nunow Shihaw.

Bw Moi naye amemuunga mkono mwaniaji wa KANU, vita vikisalia baina yake na hasimu wake wa kisiasa Dkt Ruto, wakati wanazidi kujitafutia umaarufu kabla ya 2022.

Wawili hao sasa wanaonekana kuhamisha vita vyao nje ya eneo wanalotoka, kwani kwa muda mrefu vimekuwa vikijikita katika eneo la Bonde la Ufa.

Eneo la Wajir Magharibi lina wapiga kura 27,444 waliosajiliwa kulingana na Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Tume hiyo imetangaza kuwa itatumia vituo vya upigaji kura vya kuhama hama, huku kukiwa na hofu kuwa watu wengi hawatajitokeza, kutokana na ukame ambao umelazimu familia nyingi kuhama makwao.

Maafisa wa IEBC jana walisema kuwa kila kitu kiko shwari kuendesha uchaguzi huo wa leo, mwenyekiti wake Wafula Chebukati akisema katika chaguzi ndogo zilizofanywa Ugenya na Embakasi Kusini, tume hiyo ilibaini kuwa idadi ya watu waliojitokeza ilikuwa ndogo.

Afisa mkuu wa tume hiyo Wajir Magharibi, Bw Maurice Raria, alisema tume iko na vituo 10 vya kuhamahama ambavyo vitatumiwa kuhakikisha kuwa wapiga kura waliohama kutoka ambapo walikuwa wamejisajili wanapiga kura.

“Watu watahitajika kupigia kura katika vituo ambapo walijisajili katika uchaguzi uliopita. Tumejadili hilo na maajenti na wawaniaji,” akasema Bw Raria.

Aidha, aliongeza kuwa tume haitapeperusha matokeo ya kura kutoka kwenye vituo, ila itayajumuisha katika kituo kikubwa cha eneobunge hilo.