Kunguru sasa wapokonya watu vyakula Mombasa
Na WINNIE ATIENO
SABABU za wakazi wa Mombasa kukataa matumizi ya Sh30 milioni kufukuza kunguru sasa zimeanza kuonekana, baada ya ndege hao weusi wenye kelele kuanza kuwahangaisha.
Serikali ya kaunti ya Mombasa ilikuwa imetenga kwenye bajeti kiasi hicho cha pesa ili kuwaangamiza ndege hao, ambao mbali na kelele, wakati mwingine wanaweza kummwagia mtu mizoga kwenye chakula.
Katika maeneo mengi ya wazi kunakouzwa vyakula mjini Mombasa, kunguru wamekuwa kero kubwa, kwa kuwa hata wao sawa na binadamu, huvutiwa na harufu tamu ya chakula.
Bi Fauzia Abdhallah kwa mfano anasema alipokonywa kipande cha samaki kaba hajakitia mdomoni.
Mteja wa mkahawa huo maarufu alibaki akishangaa vile alipokonywa chakula mdomoni.
“Nimepokonywa chakula jamani hawa kunguru!,” alifoka. Anapoendelea kupigwa na butwaa, familia nzima ya kunguru hao wanamiminika mezani na kubeba kilichobakishwa na mwenzao.
Hii ndio hali ambayo wateja wengi wanaozuru mikahawa ya wazi na hoteli za fuo wanapitia wanapokula milo yao.
Lakini katika hoteli ya Pride Inn Paradise na Pride Inn Flamingo, wasimamizi wamegundua namna ya kukabiliana na jinamizi hilo.
“Kunguru ni ndege mjanja sana na anajua kuotea ndio maana atatokezea kwa ghalfa anyakue chakula na huyu atoroke. Baada ya kuteseka kwa muda tukaamua kuweka vizuizi, tulichukua chupa za plastiki na kuzifanya kama vigezo, hii inamaanisha hawawezi kupepea katika mkahawa wetu,” alisema mhandisi Stephen Wambua.
Tofauti na hoteli hizo za fuoni, mikahawa mengine imeajiri vijana na kuwapa vifaa ikiwemo panda kuwadona au kuwafukuza ndege hao na hata kuwalisha ili kuwazubaisha wasisumbue wateja wao wanapo kula.
Bw Wambua ambaye ni mhadisi wa Pride Inn Paradise alisema walianza mbinu hiyo mwaka jana.
“Tunaweka chupa ambazo tunazifunga na kamba maalum za kuvua samaki na wanashindwa kupepea hadi kwa sehemu yetu ya maakuli. Walikuwa wanasumbua sana wakipepea na kwenda kuchukua chakula mezani, lakini sasa tumeweka kigezo na wanashindwa kuingia ndani. Lakini kunguru ni mojawapo ya ndege werevu sana,” alisema mhandisi huyo.
Kulingana na afisa mkuu wa muungano wa wahudumu wa hoteli tawi la Pwani Bw Sam Ikwaye kunguru ni kero kubwa sana katika kituo hicho cha utalii.
“Kunguru ni hatari huku Pwani sababu wanakula ndege wengine, kungekuwa na mbinu ya kukabiliana nayo ingesaidia sana,” alisema Bw Ikwaye.