AKILIMALI: Kongamano kuu la kilimo nchini Rwanda lawahimiza vijana kukumbatia kilimo kwa manufaa ya bara hili
INGAWA Afrika labda ndilo bara kubwa zaidi na yamkini lenye rasilimali zaidi duniani, kilimo chake kinasuasua kwa kuwa vijana hawajihusishi vya kutosha.
Kauli hii ilitolewa na wataalamu wa biashara ya kilimo waliokongamana katika jiji kuu la Rwanda, Kigali kujadili kuhusu changamoto zinazowakumba wakulima wadogowadogo barani.
Kongomano hilo lenye kaulimbiu ya Kumpa mkulima wa kawaida usemi zaidi katika mchakato wa uzalishaji na uuzaji lilibaini kwamba ingawa vijana ndio nguvukazi yenye uwezo na siha nzuri zaidi, wengi wao wametelekeza kilimo na kukimbilia mijini au kuhamia nje ya bara la Afrika hasa katika juhudi za kusaka ajira zenye tija nzuri.
Maendeleo ya kilimo yanadumazwa na idadi kubwa ya wazee wanaohusika na kilimo ilhali nguvu zao ni haba kuliko vijana.
Kongamano hilo lilidhaminiwa na shirika la utetezi la TrustAfrika, nalo lilihudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Kuvutia
Katibu mtendaji wa TrustAfrica, Dkt Ebrima Sall alisisitiza kwamba ipo haja ya kukifanya kilimo kiwavutie vijana kama chanzo cha biashara yenye tija.
Alisema hiyo ndiyo njia ya pekee ya kuondokana na utegemezi, miongoni mwa mataifa ya Afrika, wa uagizaji kutoka ng’ambo wa bidhaa muhimu.
Afisa wa mipango ya kilimo katika shirika hilo, Dkt Bethule Nyamambi alisema kwamba ni muhimu kuwahusisha wananchi wa kawaida katika ajenda ya maendeleo ili kuwezesha uwajibikaji katika sekta hiyo ya kilimo.
Aidha, kuendelea kuyagawanya mashamba katika vipande vidogo vidogo visivyoweza kuzalisha tija ni tatizo kubwa kwa ustawi wa kilimo barani.
Changamoto nyinginezo ni pamoja na ushindani katika masoko ya dunia na kukosa pembejeo za kisasa za kilimo.
Wajumbe walizitaka serikali za Kiafrika kusema kwa sauti moja katika kutetea maslahi ya wakulima wadogo wadogo ili kuwalinda kama vile serikali za Ulaya na Marekani zinavyowatetea wakulima wake.