Habari Mseto

Viongozi wazozania kipande cha ardhi mavani Thika

April 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

MASWALA ya unyakuzi wa vipande vya ardhi vya makaburi ya Thika Cemetery, yamezua utata kati ya wananchi na Kaunti ya Kiambu.

Karani anayemwakilisha Mbunge wa Thika, Bw John Mwangi, aliongoza wananchi kusitisha ujenzi wa ukuta unaojengwa kuzingira makaburi hayo.

Bw John Mwangi aliwalazimisha wajenzi wa ukuta kusitisha kazi yao akitaja kama unyakuzi usiokubalika.

“Mimi kama mzaliwa wa eneo hili la Starehe sitakubali eneo la makaburi ya umma lifanyiwe masihara ya kunyakuliwa na watu wachache wenye tamaa. Iwapo watajenga, tutaungana na wananchi kubomoa. Huo ni wizi wa wazi,” alisema Bw Mwangi.

Alisema jambo linalomkera zaidi ni kwamba mavani hapo ndipo pahala pa pekee na hutegemewa na wakazi wa Thika, na iwapo kuna watu wanaotamani kujinufaisha, “wasahau kabisa.”

 

 

Karani wa Mbunge wa Thika John Mwangi (katikati) na wajenzi wa ukuta wa kaburi la Thika Cemetery. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema ana habari ya kwamba Kaunti ya Kiambu ina nia ya kujenga vibanda kando ya ukuta wa makaburi hayo “lakini hawatafaulu.”

“Tusifanye mambo bila kufikiria maisha ya baadaye ya vizazi vijavyo. Kwa nini watu fulani wanatamani tu kutajirika na makaburi ya umma? Ni sharti tuwe na heshima na wafu ambao wamelala kwenye makaburi hayo,” alisema Bw Mwangi na kuongeza: “Mimi nitakuwa mstari wa mbele na wananchi kubomoa ukuta utakaojengwa kuzingira eneo hilo.”

Afisa mkuu wa Kaunti ndogo ya Thika, Bw Eprahim Njehe Macharia, alisema wale wanaotoa matamshi ya uchochezi kuhusu unyakuzi wamepotoka.

“Kile tunachofanya ni kujenga ukuta wa kutenganisha bayana barabara kuu na eneo makaburi. Ni nani aliye na akili timamu angetamani kunyakua makaburi?” aliouliza Bw Macharia akikanusha madai hayo.

Alisema jambo lingine linalofanya Kaunti kujenga ukuta ni kuzuia wahalifu  waliokuwa wakishuhudiwa kila mara eneo hilo lililoko karibu na Chuo Kikuu  cha Mount Kenya.

“Wahalifu wengi walizoea kujificha makaburini huku wakiwapora wanafunzi wa chuo hicho cha Mount Kenya,” alisema Bw Macharia.

Alisema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ukuta huo ukweli wa mambo utabainika.

Alisema yote yanayoshuhudiwa kwa sasa ni siasa zisizo na msingi wowote.

Naye mkazi wa mtaa wa Starehe Bi Rachael Wanjiru alisema hawatakubali ardhi hiyo ya makaburi inyakuliwe kwa sababu wazaliwa wengi wa Thika hawana eneo lingine la kuzikwa wanapotangulia mbele ya haki kama si hapo.

“Sisi kama wenyeji wa Thika hatuna pahali pa kuzika wapendwa wetu isipokuwa hapa. Wale walio na tamaa ya unyakuzi  wasahau hilo,” alisema Bi Wanjiru.

Wajenzi waliokodishwa na Kaunti ya Kiambu walisitisha ujenzi huo wa ukuta kwa muda baada ya kuogopa kushambuliwa na wananchi waliojawa na hasira za mkizi waliposikia kuhusu unyakuzi huo.