Makala

AKILIMALI: Migomba 220 ya ndizi imekuwa mbinu thabiti ya kujikimu kwake

April 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KATIKA Kaunti ya Kirinyaga, tulikutana na mkulima wa ndizi ambaye amefanya kilimo hiki kwa miaka saba sasa.

Bw Samwel Muchiri ni baba wa mtoto mmoja na mkazi wa eneo la Nyangati katika Kaunti Ndogo ya Mwea.

Ingawa yeye hukuza pia mpunga, viazi vitamu na mahindi, mmea anaoukuza kwa zaidi katika shamba lake la nusu ekari ni ndizi.

“Nimeligawa shamba langu katika vijisehemu vingi ili nikuze mimea tofauti,” anatanguliza Muchiri kwa kukiri kwamba katika sehemu ambapo ametenga ili iwe mahsusi pa kukuzia ndizi, amepanda migomba 220.

Kulingana naye, upanzi wa migomba humhitaji mkulima kuchimba mashimo yenye upana wa takriban sentimita 90 kwa kila upande na kisha kupanda miche ya ndizi huku akifukia mashimo kwa mchanga mwepesi na mbolea nyingi ya kiasili.

Baada ya upanzi huu, huwa anaanza shughuli ya kunyunyizia maji kwa wingi akitumia mifereji ili kufanikisha ukuaji wa miche kwa haraka.

Maji haya huwa anayatoa kwenye mto unaopitisha mkondo wa maji karibu na shamba lake.

Ili kuwezesha mimea hii kunawiri zaidi kwa njia bora, yeye huwa anatoa mimea na magugu yasiyohitajika kwa kutumia dawa na kadri migomba inapopata majani makubwa, huwa inaweka kivuli kote shambani ambapo pia ni njia mojawapo ya kuzuia majani yenyewe kukua kwa wingi.

Anadokeza kuwa baada ya muda, huwa anaongeza mbolea za dukani ili kuimarisha kasi ya kukua kwa migomba na uzalishaji wa ndizi.

Kwa kawaida, mgomba huchukuwa muda wa hadi miezi tisa kukomaa na kisha kumchukua muda wa miezi miwili zaidi ya kuvuna.

Kuvuna huku huwa kunafanyika mara moja kwa wiki hadi miezi miwili iishe.

Kwa mujibu wa Muchiri, kilimo hiki cha ndizi kuwa kinampa riziki ya kila siku kwani kimemwezesha kujipa ajira pamoja na kuyakimu mengi ya mahitaji yake binafsi na ya mkewe.

Kwa kawaida, migomba haina shughuli nyingi baada ya kupandwa na baadhi ya mambo ambayo huwa anafanya ni kunyunyizia maji angalau mara moja kwa wiki.

Bw Samwel Muchiri akielezea jinsi anavyotunza na kukuza ndizi katika shamba analolimiliki katika eneo la Nyangati, Mwea, Kirinyaga. Picha/ Chris Adungo

Bw Muchiri anaelezea kuwa wateja wake ni wafanyabiashara wa kati ambao hujinunulia ndizi kwa bei nafuu kabla ya kuchuuza katika masoko mbalimbali ya Kirinyaga, Nyeri, Murang’a na Nairobi kwa bei nafuu zaidi.

Katika msimu mzuri, Bw Muchiri huwa anauza kilo moja ya ndizi kwa Sh20 lakini kwa msimu wenye ushindani mkubwa kuto kwa mazao mengine haswa maembe, kilo moja ya ndizi humgharimu mnunuzi Sh14.

Anafichua kwamba mkungu mmoja wa ndizi unapovunwa, huwa na uwezo wa kutoa kati ya kilo 40 na 50 za ndizi.

Ina maana kwamba yeye hutia mfukoni kati ya Sh800 na Sh1,000 kutokana na mkungu mmoja wa ndizi.

Hata hivyo, anaungama kuwa wafanyabiashara wa kati huwa ni changamoto kubwa kwake kwani kwa kawaida, wao hutaka wanunue mazao yake kwa bei ya chini ilhali sokoni wanauza kwa bei ya juu.

Aidha, wadudu huwa ni changamoto pia na dawa za kupigana nao ni ghali mno.

Hata hivyo, anasema kilimo cha ndizi kina manufa mengi kwani baada ya kuvuna, miche mingine huchomoza na kukua na hata kustawi kama migomba mingine.

Bw Muchiri ana matumaini mengi na katika siku zijazo, anatarajia kuwa akijipelekea mazao yake sokoni ili kuepukana na wafanyabiashara wa kati ambao kwa wakati mwingine, huwadhulumu wakulima.

Jambo ambalo angeomba lifikie mashirika ya serikali na hasa Wizara ya Kilimo, ni wajue namna ya kuyashughulikia maslahi ya wakulima kwa kuandaa semina za kuwaelimisha na kuwapa ujuzi wa kisasa wa kutunza mimea na pia kupata mbegu bora ili kufanikisha
kilimo hiki cha ndizi hata zaidi.

Kaunti

Bw Muchiri pia anasema kuwa serikali za kaunti zina jukumu la kuimarisha kilimo mashinani kwani sekta hii pia ni wajibu wa gatuzi.

“Serikali za kaunti zinapaswa pia kuwavutia wawekezaji kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za ndizi ili wakulima wafaidike zaidi.”

Katika kilimo cha ndizi, Bw Muchiri mwanzo huwa anatayarisha mbegu katika sinia ili kuwezesha kukua kwa miche hadi itoe majani.

Mbegu hizi huwa ni za aina mbili, Williams na Grand Nine na ambazo huwa anaziagiza kutoka nchi ya Israeli kupitia kwa kampuni ya Aberdare Technologies.

“Baada ya mwezi mmoja katika sinia hizi, huwa ninatoa miche hii na kuiweka katika vijikaratasi ili kuiwezesha mizizi yake kukua,” anaelza.

Kulingana naye, miche hii huwa katika mazingira yenye kivuli ili kudhibiti hali ya joto inayoweza kutokana na jua.

Katika eneo hili, pia huwa anazuia kupatikana kwa wadudu na magonjwa.

Baada ya miezi miwili miche hii ikiwa katika karatasi hizi, huwa tayari kwa kuuzwa na kupandwa na wakulima wengine mbalimbali.

Wakati huu, huwa imefikisha urefu wa takriban sentimita 30 hivi.