• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:10 AM
WANDERI: Umoja ni nguzo kuu kwa wanaotetea mapinduzi

WANDERI: Umoja ni nguzo kuu kwa wanaotetea mapinduzi

Na WANDERI KAMAU

WAAFRIKA wana mengi kujifunza kutoka kwa Waarabu katika kushinikiza mageuzi ya kimfumo katika nchi zao.

Tangu 2011, nchi kadhaa za Kiarabu zimefanikiwa kuwang’atua viongozi waliokwamilia mamlakani kupitia maandamano makubwa, ambayo msingi wake mkuu ulikuwa kurejesha mfumo wa uwazi na kidemokrasia katika nchi hizo.

Kufuatia mapinduzi ya kiraia dhidi ya aliyekuwa rais wa Sudan kwa muda mrefu Omar el Bashir, kinachojitokeza ni kuwa kinyume na Waafrika wengi, Waarabu huwa na umoja wa kipekee wanapoungana kutimiza lengo fulani.

Umoja huo ndio ulishuhudiwa nchini Libya, Misri na Tunisia, katika harakati za kuwang’atua marais Muammar Gadaffi, Hosni Mubarak na Idine Ben Ali mtawalia.

Ingawa kumekuwa na dhana kuwa Muungano wa Kujihami (NATO) ndio ulichangia pakubwa katika mapinduzi ya Gaddafi, ukweli ni kuwa mapinduzi yake hayangefanikiwa bila umoja mkubwa uliodhihirishwa na raia wa nchi hiyo, ambapo wengi wao ni Waarabu.

Vivyo hivyo, mkondo huu ni changamoto kubwa kwa Waafrika kufahamu kuwa bila umoja, watabaki kulia na kulalamika kutokana na mtaasisiko wa tawala za kiimla katika nchi zao.

Kwa utathmini wa kina wa hali ilivyo duniani, ni wazi kuwa nchi nyingi zilizo na marais waliokwamilia mamlakani kwa miongo na miongo ni za watu ambao karibu wote ni Waafrika.

Barani Afrika, marais Yoweri Museveni (Uganda), Dennis Sassou Ngueso (Congo Brazaville), Paul Bbiya (Cameroon) kati ya wengine wamekatalia mamlakani kabisa.

Baadhi yao wameziongoza nchi hizo kwa zaidi ya miongo mitatu—kumaanisha kuwa kuna kizazi kizima kilichopo ambacho hakimfahamu kiongozi yeyote isipokuwa wao.

La kushangaza ni kuwa, viongozi hao wanafanya kila juhudi kuwanyamazisha wale ambao wanaoonekana kuamka na kupinga tawala zao dhalimu—kama ambavyo Bw Museveni amekuwa akimhangaisha mwanamuziki Bobi Wine.

Kenya vile vile haijaachwa nyuma kwani imegeuzwa “falme ndogo” ya familia za rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta na makamu wake wa kwanza, Jaramogi Oginga Odinga.

Kwa zaidi ya miaka 50 baada ya kujinyakulia uhuru mnamo 1963, Kenya bado imegawanyika katika makundi mawili makuu ya kisiasa—linalomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta (mwanawe Mzee Kenyatta) na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, mwanawe Jaramogi.

Kwa kutumia ujanja na uzoefu wao wa kisiasa, sasa wamewatia Wakenya kapuni kupitia “muafaka wa kisiasa kati yao” ili kuzima maasi yoyote yanayopinga uongozi wao.

Hadaa iliyopo ni kuwa “nchi imetulia.” Ni lazima Waafrika wajifunze kutoka kwa Waarabu kuwa ni sharti waungane kwanza na kutambua changamoto zinazowaathiri.

Ni lazima kizazi kilichopo kijifunze kutoka kwa kizazi cha mababu zetu ambao waliondoa tofauti zao zote na kuungana kumpiga vita mkoloni kupitia Vita vya Ukombozi vya Mau Mau.

Ndivyo kizazi cha pili cha wanasiasa wakongwe kama Koigi wa Wamwere, James Orengo na wengine kilipoungana kuupigania Ukombozi wa Pili wa Kisiasa kutoka kwa Kanu.

La sivyo, wimbo wa “udikteta, dhuluma na ukandamkizaji” utaendelea kuwa vinywani vya Waafrika.

[email protected]

You can share this post!

MUTANU: Juhudi zifanywe kukabili mabadiliko ya hali ya anga

MBURU: Mazoea ya serikali kulazimishia wananchi mambo...

adminleo