• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Wanafunzi wa siasa za Moi wakusanyika Kabarak kuzika mwanawe

Wanafunzi wa siasa za Moi wakusanyika Kabarak kuzika mwanawe

Na PETER MBURU

MAZISHI ya Jonathan Toroitich Moi aliyezikwa Jumamosi, yaliwaleta pamoja wanasiasa waliokuzwa kisiasa na baba yake Rais mstaafu Daniel Moi.

Viongozi waliohudhuria ibada katika chuo kikuu cha Kabarak, akiwemo Naibu Rais William Ruto, walimmiminia sifa Mzee Moi kwa kuwalea kisiasa.

Japo Mzee Moi hakuhudhuria hafla hiyo, watu aliwaingiza katika siasa kutoka kote nchini walimshukuru kwa kuwajenga. Takriban viongozi wote waliopata fursa za kuhutubu walimshukuru wakisema aliyewafanya kufika waliko sasa.

Naibu Rais alimbukumbu YK92, vuguvugu la vijana lililokuwa likimpigia kampeni Mzee Moi mnamo 1992, ambalo waliliongoza pamoja na mbunge wa zamani wa Lugari Cyrus Jirongo ambaye pia alihudhuria hafla hiyo.

“Rais Moi ana watoto wengi, wa kibaiyolojia na wengine wetu ambao tulilelewa naye. Na tumekuja hapa kama watoto wa Rais Moi kumzika ndugu yetu,” akasema Dkt Ruto.

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi alisema familia yake na ile ya Mzee Moi zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka mingi, akimsifu Rais huyo mstaafu kuwa kielelezo chake na cha wengi kisiasa.

Seneta wa Bungoma Moses Wetangula vilevile hakuchelea kumkumbuka Mzee Moi, akisema “Mimi ni mmoja wa wale walilelewa kisiasa na Mzee Moi, aliniteua bungeni 1993 na hapo ndipo safari yangu kisiasa ilianza hadi leo.”

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye aliwakilisha Baraza la Magavana (CoG) alisema Rais huyo Mustaafu ndiye alimpa kazi kwa mara ya kwanza.

“Mimi ni mmoja wa wale walipitia katika mabega ya Rais Mstaafu. Nilimjua kupitia Isaac Salat, babake Nick Salat, ambaye alinifanya kupewa kazi na Mzee Moi hata nilipokuwa mbunge Butere, hadi nilipo sasa,” akasema Bw Oparanya.

Aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto alisema: “Mimi kama viongozi wengine hapa tulilelewa na Mzee Moi. Ndio maana hata naona haya kuongea kwa boma lake. Mimi ni mmoja wa wale aliowateua kuwa mawaziri tukiwa vijana sana, tulipoingia siasa.”

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alikiri kwamba alikuzwa kisiasa na Mzee Moi.

You can share this post!

Kuria sasa asajili TNA

Kidero alia EACC ilimnasa kimakosa

adminleo