MakalaSiasa

JAMVI: Je, Uhuru anamuandaa Gideon Moi?

April 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta amekuwa akionyesha heshima ya kiwango cha juu kwa Rais Mustaafu Daniel Moi pamoja na familia yake, hasa mwanawe Rais huyo wa zamani-seneta wa Baringo Gideon Moi.

Kila kunapokuwa na jambo kwa familia ya Mzee Moi, Rais hachelei kutuma jumbe za kufariji familia hiyo, na pia kuwatembelea nyumbani kwao Kabarak.

Rais Kenyatta aidha amekuwa na uhusiano wa karibu na seneta Moi, ambaye wameonyesha kuheshimiana sana na hata ingawa hawazungumzi mengi mbele ya umma, lugha zao za ishara zikionyesha kuwa uhusiano baina yao ni wa karibu sana. Katika ziara za Rais Kabarak, ni seneta Moi ambaye humpokea na kuwa katika vikao wanavyofanya na Mzee Moi.

Kando na Rais Kenyatta, viongozi wengine kama wa chama cha ODM Raila Odinga, wa Wiper Kalonzo Musyoka, Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli, Gavana wa Mombasa Hassan Joho miongoni mwa wengine wamekaribishwa nyumbani kwa Mzee Moi Kabarak kumwona.

Lakini kwa kinaya, Naibu Rais William Ruto-ambaye ni hasimu mkubwa kisiasa wa seneta Moi-amekuwa akizuiwa kuingia nyumbani kwa Rais huyo mustaafu Kabarak, kwa sababu zinazoaminika kuwa za kisiasa.

Wakati Rais Kenyatta alipotembea Kabarak mara ya kwanza, walikuwa wakishiriki hafla pamoja na Dkt Ruto katika mazishi ya mkewe aliyekuwa afisa mkuu wa jeshi Joseph Kasaon, lakini hakuandamana naye nyumbani kwa Mzee Moi.

Baadaye alipojaribu kwenda kumwona, Naibu Rais alizuiwa, akiambiwa kuwa Mzee Moi alikuwa akifanyiwa matibabu na hangeweza kumwona yeyote.

Baadaye, wandani wake walimkashifu seneta Moi kuwa alimzuia Dkt Ruto kuonana na babake.

Uhusiano baina ya Rais na Bw Moi umefanya wadadisi kuhisi kuwa kuna uwezekano huenda anawazia ‘kumrudishia mkono’ kutokana na hatua ya babake mnamo 2002, alipompendekeza kuwania Urais, wakati hakuwa anajulikana kisiasa.

“Kuna kila ishara kutokana na matendo fulani anayofanya Rais, kuwa huenda akampendekeza Bw Moi. Huenda akawa anataka kurudisha mkono kulipia jinsi Rais Mustaafu Moi alimuinua mnamo 2002 kwani ni hatua hiyo iliyompa msingi wa kuwa Rais miaka 10 baadaye,” anasema Gilbert Kabage.

Bw Kabage anaongeza kuwa, matamshi ya Rais mwaka jana kuwa chaguo lake la mwaniaji katika uchaguzi ujao litashangaza watu hayawezi kupuuziliwa, suala hili linapowaziwa.

Itakumbukwa kuwa seneta Moi pia amekuwa na uaminifu mkubwa kwa Rais kwani hata katika uchaguzi wa 2017, chama chake cha KANU kilikosa kuwasilisha mwaniaji Urais ili kuungana na Jubilee kumuunga mkono Bw Kenyatta.

Japo nyakati zote wamekuwa wakitofautiana na Naibu Rais, seneta Moi amekuwa akisisitiza kuwa wanamuunga mkono Rais Kenyatta, na hata katika hafla moja eneo la Rongai mwaka jana akasema kuwa Rais hafai kusumbuliwa kuhusu atakayemuunga mkono 2022, kwani “wakati huo ukififa anajua atakavyofanya na sina shaka na hilo.”

Katika vita vya ubabe baina ya Bw Moi na Dkt Ruto Bonde la Ufa vilevile, Rais Kenyatta anaonekana kuwa na uhusiano mzuri na viongozi wandani wa Bw Moi, ikilinganishwa na wale wa Dkt Ruto ambao uhusiano unazidi kuwa baridi.

Hali ya Rais kutoweka wazi jinsi alikuwa akifanya katika muhula wake wa kwanza kuhusu ikiwa atamuunga mkono naibu wake katika uchaguzi ujao licha ya wandani wa Dkt Ruto kuuliza hivyo mara kwa mara imeonyesha kuwa mambo yote si sawa.

Akiwa mjini Eldoret wakati wa kampeni mwaka jana, Rais aliambia wakazi “Tumalize hii miaka mitano jameni mimi niende nipumzike, Ruto ashikilie asukume huko mbele, dunia hiyo iendelee” matamshi ambayo alikuwa akiyarejelea mara kwa mara, lakini tangu achaguliwe yamempotea.

Vilevile, kumekuwa na matukio ambapo seneta Moi aidha amehudhuria hafla kubwa za serikali ama kufanya vikao na Marais wa mataifa jirani na maafisa wengine wakuu, watu wakishangaa alikuwa akizungumza nini nao na kama nani.

Kwa mfano, Bw Moi wiki kadha zilizopita alikutana na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kusema kuwa walijadili masuala ya uongozi, kisha Rais wa Uganda Yoweri Museveni alipokuwa nchini akatembea nyumbani kwa Mzee Moi Kabarnet Gardens, Jijini Nairobi.

Museveni alikuwa nchini kwa ziara rasmi, lakini akatenga wakati “kumtembelea na kumjulia hali rafikiye mzee kwa kuwa wamejuana na kuwa marafiki kwa miaka mingi,” seneta Moi akasema.

Wakili Bernard Ngetich anahoji kuwa Rais Kenyatta anaonyesha kuwa na uaminifu kupita kiasi kwa seneta Moi, hali inayoibua wazo kuwa huenda mchezo wa 2022 tayari umecheezwa na sasa anaandaliwa tu.

“Familia ya Rais na ya Mzee Moi zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa muda mrefu na Rais anaonekana ana nia ya kuuendeleza. Huenda ziara zake zinalenga kumjenga seneta Moi na kutoa ishara kwa watu kuhusu mahali ‘baraka zake’ ziko,” anasema wakili huyo.

Jumatatu wiki hii, Rais alikuwa nyumbani kwa Mzee Moi Kabarak kumfariji, baada ya mwanawe Jonathan Toroitich kuaga dunia wiki iliyopita.

Katika ziara hiyo, Rais aliahidi familia ya Mzee Moi msaada wa serikali katika shughuli zote za kumuaga mwendazake, na kusisitiza kuwa walikuwa wakiomboleza pamoja.

Kama kawaida, katika ziara hiyo alipokelewa na seneta Moi, ambaye alikuwa na viongozi wanaomuunga mkono kama Gavana wa West Pokot John Lonyangapuo, mbunge wa Tiaty William Kamket, aliyekuwa mbunge wa Eldama Ravine Musa Sirma, Katibu Mkuu wa KANU Nick Salat, pamoja na wengine.

Hata hivyo, alipoenda kutoa rambirambi zake Jumatano, Dkt Ruto alienda nyumbani kwa marehemu eneo la Eldama Ravine badala ya Kabarak kama Rais, madai yakiibuka kuwa alikuwa amejaribu kwenda Kabarak, lakini akazuiwa akiambiwa kuwa maombolezi yalikuwa yakifanyikia Eldama Ravine.