• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Polisi wasaka genge hatari linalohusishwa na wanasiasa

Polisi wasaka genge hatari linalohusishwa na wanasiasa

Na ERIC MATARA

MAAFISA wa usalama wameanzisha msako dhidi ya genge hatari la wahalifu ambalo limekuwa likihangaisha wakazi wa Nakuru, haswa katika maeneo ya mabanda.

Wakazi wa eneo hilo wanahusisha genge hilo na wanasiasa wawili kutoka eneo la Nakuru. Inadaiwa kuwa wanasiasa hao wanafadhili shughuli za genge hilo.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa genge hilo ni miongoni mwa magenge 90 yaliyoharamishwa na aliyekuwa waziri wa usalama marehemu Joseph Nkaissery mnamo 2016.

“Sote tunafahamu kuwa wanasiasa wawili wanafadhili genge hilo. Vijana wa genge hilo wanapokamatwa, wanasiasa hao hujitokeza na kuwatoa kwa dhamana,” akasema mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyeomba jina lake libanwe.

Kulingana na wakazi, wanasiasa hao hutumia vijana wa magenge hayo kutishia wapinzani wao haswa wakati wa uchaguzi.

Watu waliohojiwa walisema genge hilo limekuwa likifadhiliwa na wanasiasa hao kwa takriban miaka saba.

“Kundi hilo huwa miongoni mwa kikosi cha kuendesha kampeni za wanasiasa hao. Genge hilo lilitumiwa na wanasiasa hao katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017 kutishia wapinzani wao,” akasema mkazi.

Kulingana na polisi, genge hilo limejihami kwa mapanga, visu na hata bunduki.

Polisi pia wanaamini kwamba genge hilo limekuwa likilindwa na wanasiasa wenye ushawishi.

Polisi pia wanashuku kuwa genge hilo pia limekuwa likitumiwa na walaghai kuibia watu fedha kwa njia ya simu katika maeneo ya Nakuru.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa genge hilo lenye wanachama kati ya 10 na 20 linaendesha shughuli za uhalifu katika maeneo ya Kivumbini, Lake View, Kwa Rhoda, Kaptembwa, Flamingo, Kaloleni na Bondeni.

Wahalifu hao wameweka kibanda cha kuwasaidia watu kutatua matatizo yanayohusiana na kutuma au kupokea fedha kwa njia ya simu.

Ni katika kibanda hicho ambapo huwalaghai watu na kuwaibia fedha zao kwa njia ya Mpesa au Airtel Money.

Miongoni mwa arafa ambazo hutumwa na genge hilo kwa waathiriwa ni: “Hello mummy! nimekosea nikakutumia pesa. Tafadhali nirudishie hizo pesa, kwa sababu nilikuwa namtumia mamangu ambaye ni mgonjwa.”

You can share this post!

Waumini wa ACK wakataa uteuzi wa viongozi wapya jimbo la...

Kioja waombolezaji wakiachiwa mwili Likoni

adminleo