• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Kaunti za Nakuru na Baringo zaungana kukabili kolera

Kaunti za Nakuru na Baringo zaungana kukabili kolera

NA RICHARD MAOSI

Wahudumu wa afya kutoka kaunti ya Nakuru wameweka mikakati ya kukabiliana na mkurupuko wa maradhi ya kolera yaliyoripotiwa kuzuka wiki iliyopita.

Kulingana na mkuu wa afya ya umma Samwel King’ori, watu watatu walikuwa wametibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani kufikia Ijumaa.

“Wengine wawili wanaendelea kupokea matibabu huku mmoja akilazwa ili kufanyiwa uchunguzi zaidi,” alisema.

King’ori aliongezea kuwa maafisa wake walikuwa mashinani,hasa katika maeneo ya Kaptembwa, Rhonda na Freearea ambayo visa hivyo vilikuwa vimeripotiwa kuzuka.

Aidha aliwahakikishia wakazi kuwa vituo vya afya vilikuwa na dawa za kutosha, na hapakuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi.

Maji haya machafu kutokana na mvua ni hatari kwa matumizi ya binadamu. Picha/ Richard Maosi

Baadhi ya Hospitali ambazo ziko macho ni Pamoja na Nakuru Level Five,Langalanga,Mogotio,St Mary na ile ya Naivasha.

Wakazi wameombwa kula chakula na matunda safi. “Wajiepushe na vyakula vya kuchuuza barabarani visivyozingatia usafi wa hali ya juu,”alisema.

Na katika kaunti jirani ya Baringo hali ni kama hiyo,ambapo swala la uchafuzi wa mito limeripotiwa kuwapatia wakazi hofu.

Wanalaumu wachuuzi wanaoteka maji mitoni na kusafirisha hadi kwenye maeneo ya kufanyia biashara,kama vile mikahawa bila kuzingatia usafi .

Alfred Kiarie kutoka Molo River anasema ingawa serikali imetoa ilani kali kwa wachuuzi wa maji bado baadhi yao wanasomba maji kutoka mtoni wakitumia punda na pikipiki.

Ingawa mito yenyewe imejaa takataka,za kila aina huku nyingine zikielea juu ya maji.

Mto Molo ni sugu kwani waendeshaji pikipiki wamekuwa wakitoa maji hapa na kusafirisha hadi kwenye mitaa inayozunguka eneo la Eldama Ravine.

Taka nyingine hutoka kwenye ploti za kukodisha na humwagwa mtaroni kabla ya kuelekezwa na maji ya mvua mitoni.

Raia wanahimizwa kunywa maji safi. Picha/ Richard Maosi

“Mara ziingiapo ndani ya mto huchanganyika na maji,na kuzua maradhi ya kuambukiza kama vile kipindupindu na cholera,”alisema.

Bi Sheila Wamboi anaona kama serikali ya kaunti ya Baringo imewadharau wakazi ,waliowapigia kura.

Anasema hakuna mahali pa kuhifadhi taka wala hajawai kuona usimamizi wa afya kutoka kaunti ya Baringo ukikagua hali ya usafi kwenye maeneo ya kufanya biashara..

“Uhifadhi wa maji ni jukumu letu sote,bila hivyo maradhi mbalimbali yanaweza kutokea.Licha ya uvundo mkali kutoka mtoni bado wachuuzi wanaendelea kuteka maji waziwazi,”alisema.

Wakaazi hao wanaomba wizara ya afya ya Kaunti ya Nakuru na Baringo,ikishirikiana na wahifadhi wa mazingira,kuhakikisha wale wanaochafua mito wanachukuliwa hatua kali.

Kaunti nyingine zilizoadhirika na Cholera ni Pamoja na Naivasha,Nyeri na Nairobi.

You can share this post!

Menengai Oilers mabingwa wa Great Rift Top Fry 10 Aside

Afisa aisifia Safaricom kuandaa kipute cha Chapa Dimba

adminleo