HabariSiasa

Kuria akaangwa kusajili TNA

April 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na NDUNGU GACHANE

MAGAVANA wawili na wabunge wanne wa Mlima Kenya wamemshutumu vikali Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria kwa kubuni chama kipya ili kumrithi Rais Uhuru Kenyatta, kama kiongozi wa kisiasa wa ukanda huo.

Magavana Ann Waiguru (Kirinyaga), Mutahi Kahiga (Nyeri), Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a) wabunge Peter Kimari (Mathioya), Ndindi Nyoro (Kiharu) na Kimani Ichung’wa (Kikuyu), walisema kuwa hatua ya Bw Kuria inairejesha nchi katika enzi ya vyama vya kisiasa vya kikabila.

Bw Kuria amebuni chama kipya cha Transformational National Alliance (TNA)) ambacho tayari ashakisajili kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Viongozi hao walisema kuwa ukanda huo utabaki katika Chama cha Jubilee (JP) kilichobuniwa na Rais Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Viongozi hao walimshauri Bw Kuria kuacha chama hicho na kurudi katika Jubilee ili asihatarishe safari yake ya kisiasa.

Bw Kang’ata alisema ikiwa Bw Kuria analenga kuwania urais, basi anapaswa kuacha chama chake na kushiriki katika uchaguzi wa mchujo akitumia chama hicho chake.

“Bw Kuria anapaswa kuacha chama chake na kurudi Jubilee ili kuwaeleza viongozi wengine maono na nia yake ya kutaka kuwania urais. Ikiwa hatafanya hivyo, basi anahatarisha mustakabali wake wa kisiasa,” akasema.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bi Waiguru alisema: “Si vyema kubuni chama cha kikanda wakati nchi inaanza kukumbatia vyama vinavyoleta umoja wa kitaifa.”

Alisema Jubilee itahimili mawimbi ya kisiasa kwenye siasa za urithi wa Rais Kenyatta hapo 2022, kwani hali hiyo ni ya kawaida katika chama chochote cha kisiasa.

Gavana Kahiga alipuuzilia mbali hatua ya Bw Kuria, akitilia shaka ikiwa ashawahi kushiriki katika uchaguzi wowote wa kitaifa wenye ushindani, ndipo akapata ujasiri wa kubuni chama hicho.

“Je, Bw Kuria ashawahi kushiriki katika siasa zozote zenye ushindani? Alipata wadhifa wake kama mbunge bila ushindani wowote. Ninashangaa alikotoa ushujaa wa kubuni chama anachodai kinaliwakilisha eneo la Mlima Kenya. Jubilee ingali chama maarufu na kinachopendwa zaidi katika ukanda huu,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Ichung’wa, ambaye ni mwanachama wa kundi la TangaTanga ambalo linamuunga mkono Dkt Ruto, alimlaumu vikali Bw Kuria kwa kupanga njama za kusambaratisha ufanisi ulioletwa na serikali ya Jubilee.

“Mpango huo ni njama ya kurudisha nyuma nchi, kufuatia ufanisi tuliopata. Lengo lake ni kuturejesha katika enzi ya chuki za kikabila,” akasema. Aliapa kutounga mkono chama hicho.

Bw Nyoro alimtahadharisha Bw Kuria kuhusu athari za kisheria za kubuni na kuunga mkono chama pinzani cha kisiasa kinyume na kile alicho mwanachama wake.