Habari MsetoSiasa

Nanok aomba chakula cha kuvutia watu kujisajili Huduma Namba

April 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY LUTTA

GAVANA wa Turkana Josphat Nanok ameitaka serikali ya kitaifa kuwapa wakazi wa eneo hilo chakula cha msaada ili kuwawezesha kujitokeza kujisajili kwa ajili ya Huduma Namba.

Wakazi zaidi ya 609,167 wanahitaji chakula cha msaada kwa dharura katika wadi zote 30 za Kaunti ya Turkana.

Bw Nanok ambaye Jumamosi alizunguka katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo kutoka Lodwar hadi eneo la Kibish lililoko katika mpaka wa Kenya na Ethiopia kuchunguza hali ya ukame, alisema kuwa chakula cha msaada ndicho kitawezesha wakazi kujitokeza na kujisajili kupata Huduma Namba.

“Nawahimiza wakazi wa kaunti hii kujitokeza na kujisajili kwa ajili ya Huduma Namba, lakini naitaka serikali ya kitaifa kuwapa chakula cha msaada ili kuwavutia,” akasema Gavana Nanok.

Kenya tayari imetuma machifu kutoka Turkana kuenda nchini Uganda kuwashawishi wachungaji 40,000 waliovuka mpaka kutafutia mifugo wao malisho, kurejea nyumbani na kujisajili.

Wakati wa ziara yake, Gavana Nanok alizungumza na wakazi wa maeneo ya Lolupe, Losajait (Wadi ya Nakalale); Kankurdio, Kaeris katika Wadi ya Kaeris; Kaaleng, Ekicheles, Nakinomet katika Wadi ya Kaaleng/Kaikor na Wadi ya Kibish ambayo imeathiriwa pakubwa na wizi wa mifugo unaotekelezwa na watu kutoka jamii ya Nyangatom kutoka nchini Ethiopia.