WANDERI: Dini ina nafasi muhimu kwa jamii, ilindwe vilivyo
Na WANDERI KAMAU
NI dhahiri kuwa maabadi yoyote ni pahali patakatifu ambapo panapaswa kuheshimiwa.
Licha ya tofauti nyingi zilizomo miongoni mwa dini mbalimbali duniani, utakatifu wa maabadi huwa mmoja—lengo lake kuu huwa ni kumheshimu Mwenyezi Mungu.
Mungu wa Wakristo, Waislamu, Wahindi, Wabuddha kati ya dini zingine huwa mmoja, licha ya utofauti mkubwa uliopo katika ufasiri wake.
Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka mijadala ya inayowalaumu baadhi ya viongozi wa kidini nchini kwa kuwaruhusu wanasiasa kutumia maabadi kama majukwaa ya kuendeleza siasa zao.
Lawama hizo zinaelekezewa makanisa. Viongozi wanalaumiwa kuwa kutowadhibiti wanasiasa wanapohudhuria misa ama ibada katika makanisa yao—ambapo huzitumia kama majukwa ya kusema lolote walitakalo bila kumwogopa yeyote.
Kando na hayo, makanisa pia yanalaumiwa kwa kuwa majukwaa ya ulanguzi wa pesa; wanasiasa wanadaiwa kutoa michango mikubwa mikubwa bila makanisa kuuliza asili yake.
Ingawa huu ni mjadala ambao umekuwepo kwa muda mrefu, unaibua maswali mengi kuhusu nafasi ya dini katika jamii ya sasa.
Je, ushawishi wa dini ungalipo? Mbona viwango vya maadili vimedorora sana licha ya uwepo wa viongozi wa kidini? Jamii imemsahau Mungu? Dini ingali ina nafasi yake kweli?
Kimsingi, haya ni maswali mazito, ingawa ni vigumu kuyajibu. Ni maswali yanayoibua mdahalo mzito ambao unapaswa kuendeshwa kwa pamoja na kila mwanajamii.
Urejeleo wa kina wa historia unaonyesha kuwa kinyume na jamii ya sasa, jamii za zamani zilichukulia masuala ya dini kwa uzito sana.
Aghalabu, kulikuwa na adhabu kali kwa wale ambao wangekaidi taratibu, kanuni na miiko iliyowekwa kuhusu jamii hizo.
Kwa mfano, katika falme kongwe kama Ugiriki, Cartharge, Roma kati ya zingine, dini ilikuwa mojawapo wa dira kuu zilizozipa jamii hizo mwelekeo kuhusu masuala mbalimbali yaliyozihusu.
Dini ilikuwa yenye uzito mkubwa kiasi kuwa wafalme na watawala wa falme hizo waliteuliwa na kutawazwa kwa kuzingatia kanuni zilizojikita katika dini.
Falme hizo pia zilizingatia semi za miungu mbalimbali walioheshimiwa sana.
Katika falme ya Ugiriki, mungu Athena ndiye aliyekuwa mwenye usemi mkuu kuhusu mustakabali wa falme hiyo na mahusiano yake na falme jirani.
Miungu hao pia walikuwa na wataalamu ambao wangeeleza wakati wamefurahi ama wamekasirika.
Hali yao iliashiria nyakati tofauti tofauti kuhusu mustakabali wa jamii hizo. Walipocheka—licha ya kutokuwa viumbe hai—hilo liliachilia baraka kwa jamii ama falme husika. Walipolia, iliachilia mkosi ambao ungeikumba jamii.
Kwa hivyo, miungu hao walitekeleza majibu muhimu katika ulainishaji wa maadili miongomi mwa kila mwanajamii.
Kwa hayo, imefikia wakati ambapo jamii ya sasa inapaswa kukoma kukwepa kanuni za kidini zinazopaswa kuzingatiwa kuwakosoa wanasiasa wanaovamia na kuharibu dhima ya maabadi.
Lazima watetezi wa ukweli wasimame na kutetea utakatifu wa dini dhidi ya uvamizi wa watu wasiojali athari za matendo yao kwa jamii.